'TUNAVUNA VIAZI MAGUNIA 150, MPUNGA 40 KWA EKARI’


Mkulima kutoka Kata ya Luponde mkoani Njombe,
Neema Mgaya, akionesha mbegu bora ya viazi mviringo kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Na Nora Damian, Mbeya
 
Wakulima wa mpunga na viazi katika Mikoa ya Njombe na Mbeya wameongeza uzalishaji wa mazao kutoka magunia 15 hadi 40 kwa ekari moja ya mpunga na 150 kwa viazi.
 
Mafanikio hayo ni baada ya kupata mafunzo kutoka katika Mpango wa Kukuza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) ambao ni ubia kati ya seta ya umma na binafsi unaolenga kuchochea uwekezaji kwenye kilimo biashara katika ukanda huo.

Wakulima hao ni Atufena Mbembati kutoka Skimu ya Madibila Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya anayelima mpunga na Neema Mgaya mkazi wa Lusitu Kata ya Luponde mkoani Njombe anayelima viazi mviringo na parachichi.
 
Wakizungumza Agosti 7, 2023 na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, wamesema kilimo kimebadilisha maisha yao na familia zao.


Atufena Mbembati (kushoto) kutoka Skimu ya Madibila Wilaya ya Mbarali, akionesha mbegu ya mpunga kwa wananchi waliotembelea banda lao kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
 
“Nilikuwa nalima kilimo cha mazoeya, situmii mbolea, nilikuwa napanda mbegu za kienyeji, lakini tangu ilipokuja mbegu ya kisasa kuna mafanikio. Sagcot inatusaidia kwa mambo mbalimbali, kutupatia mafunzo, tumekuja Nanenane kujifunza wametugharamia kwa manufaa yetu,” amesema Atufena Mbambati.
 
Amesema alianza kulima mpunga mwaka 1997 akiwa na ekari moja na kuvuna magunia 15 lakini kwa sasa ana ekari tano ambapo huvuna magunia 40 kwa kila ekari.
 
Amesema mafanikio mengine aliyoyapata ni kununua mashine ya kulimia (Power tiller) kwa Sh milioni 12, kujenga nyumba mbili ambapo moja amepangisha na nyingine anayoishi.
 
“Mimi ni mjane lakini sijawahi kufeli maisha, maisha yanaendelea, walitufundisha tusiuze mpunga, tunakoboa tunauza mchele kwa faida,” amesema.
 
Aidha amesema pia wamejiunga kwenye Kongani ya Mbarali ya uandaaji wa mbegu na tangu mwaka jana wameanza kuuza ambapo gunia moja huuza Sh 150,000.
 
Naye Neema amesema analima ekari tano za viazi mviringo na kuvuna magunia 150 kwa ekari ambayo yameongezeka kutoka 30 ya awali kabla ya kupata mafunzo na kutumia mbegu bora.
 
“Sagcot wametuwezesha kwenye mashamba darasa na kutuletea mbegu. Kilimo hiki kimenisaidia sana, nasomesha watoto, nimejenga nyumba.
 
“Wakulima wasikilize ushauri wa wataalam, wapime udongo ili kujua aina ya mbolea inayotakiwa,” amesema Neema.





Powered by Blogger.