CHUTCU WAZALISHA KILO MILIONI 8 ZA TUMBAKU

Mashamba ya tumbaku yaliyopo Chunya Mkoa wa Mbeya.

Na Nora Damian, Mbeya

Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku Chunya (CHUTCU LTD) kimeuza zaidi ya kilo milioni 8.7 kwa thamani ya Dola milioni 16.5 katika msimu wa mwaka 2021/22.

CHUTCU kilichoanzishwa mwaka 2000 ni muungano wa vyama vya ushirika vya msingi vinavyolima zao la tumbaku Chunya na Songwe pamoja na mazao ya chakula.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 4, 2023 Meneja Mkuu wa CHUTCU, Christian Msigwa, amesema wastani wa bei katika msimu huo ilikuwa Dola 1.83 ambapo wakulima walipata zaidi ya Sh bilioni 6.9.

Amesema wamekuwa wakiwatafutia wakulima masoko, pembejeo na kuwapa elimu ya zao hilo na ushirika.

“Tunao wataalam wanaotoa elimu kuanzia hatua za awali za uandaaji wa kitalu, kupanda shambani na tunatafuta masoko na makampuni mbalimbali yanayonunua tumbaku, sasa hivi tuna kampuni tatu zinazonunua tumbaku,” amesema Msigwa.

Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku Chunya, Christian Msigwa, akizungumza kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Amesema shughuli za chama hicho ni kustawisha hali ya wanachama wake kwa kuendesha shughuli za kilimo zinazoendeshwa na vyama pamoja na wanachama wake kwa kufuata misingi na taratibu za vyama vya ushirika.

Amesema wamekuwa wakala wa kukusanya, kuhifadhi pamoja na kutafuta soko la mazao ya tumbaku, alizeti, mahindi, korosho na mengine kwa lengo la kuyauza kwa bei nzuri kwa faida ya wanachama.

Pia wamekuwa wakinunua na kuuza pembejeo za kilimo kwa wanachama wake kwa bei nafuu ili kuboresha mazao ya biashara na chakula.

Chama hicho kinatoa elimu ya ushirika kwa wanachama wake na kuwaendeleza kielimu watendaji wake.

“Tumeanzisha na kuendeleza mitandao mizuri na imara ya kilimo bora cha tumbaku na mazao mengine, pia tumeanzisha viwanda vidogo vidogo na vikubwa,” amesema Msigwa.



Powered by Blogger.