CRDB YAMKOSHA RAIS SAMIA


Rais Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa Benki ya CRDB, Maregesi Shaaban, alipotembelea banda la benki hiyo katika kilele cha maadhimisho ya Nanenane kitaifa jijini Mbeya. Wengine Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Ofisa Mkuu wa Fedha wa wa benki hiyo, Fredrick Nshekanabo.


Na Nora Damian, Mbeya

Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa mikopo katika sekta ya kilimo na kuwataka wakulima kuongeza juhudi za uzalishaji ili kutosheleza mahitaji ya ndani na kulisha mataifa mengine.

Kwa miaka mitano benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya Sh trilioni 3.9 sawa na asilimia 49 ya mikopo yote iliyotolewa na benki kwenye sekta ya kilimo na mifugo nchini.

Rais Samia ametoa pongezi hizo leo Agosti 8, 2023 baada ya kutembelea benki hiyo kwenye kilele cha Maonesho ya Wakulima Nanenane viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

“Nimeona mabenki yalivyochangamkia fursa za kilimo, ufugaji na uvuvi, kuna mikopo ambayo mabenki yanatoa kwa wakulima, wavuvi na wafugaji.

“Nishukuru sana mabenki, kila benki imejitoa inakwenda kule vijana waliko kuwafundisha mambo ya biashara, matumizi ya fedha kwenye mradi na jinsi ya kufanya faida,” amesema Rais Samia.

Aidha ameitaka benki hiyo kuendelea kufuatilia zana za kilimo wanazowakopesha wakulima na kuwasaidia kutengeneza pindi zinapoharibika.

Amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya mikopo, ruzuku, bima, huduma za ugani na nyingine hivyo ni jukumu la wakulima kuzalisha kwa wingi ili kulisha ndani na mataifa mengine.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara katika Benki ya CRDB, Maregesi Shaaban, amesema kwa kushirikiana na wauzaji wa vifaa vya kilimo (Agricom) wametoa mikopo ya Power Tiller kwa baadhi ya wakulima wa mpunga mkoani Mbeya.

“Tutaendelea kushirikiana kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya kilimo unatamalaki kwa ndani na nje ya nchi,” amesema Shaaban.

Kwa mujibu wa mkuu huyo, wakulima zaidi ya 600 wanatarajiwa kukopeshwa matrekta, power tiller, zana za kuvunia na fedha za kununua pembejeo ikiwemo mbegu, mbolea na madawa.

Amesema pia wameiongezea mtaji wa Sh bilioni 10.2 Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) na Sh bilioni 7 kwa Benki ya Ushirika Tandahimba (TACOBA) na sasa zinajiendesha kwa faida.

Mmoja wa wakulima wa mpunga kutoka Mbarali aliyepatiwa mkopo wa zana za kilimo, Halima Ally, amesema zitamuwezesha kuendeleza uzalishaji.

“Tunaishukuru Crdb na Agricom tumepata power tiller, sasa tutaacha kulima kwa jembe la kutumia ng’ombe,” amesema Halima.



 


Powered by Blogger.