DMI KUFUNGUA MATAWI MWANZA, LINDI

Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Dk. Tumaini Gurumo, akizungumza kuhusu huduma wanazozitoa kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.


Na Nora Damian, Mbeya

Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kinatarajia kufungua matawi katika Mikoa ya Lindi, Mwanza na Kigoma ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Kwa sasa chuo hicho kina wanafunzi wa kozi ndefu 3050 na 6,000 wa kozi fupi za ubaharia.

Akizungumza kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, Mkuu wa chuo hicho, Dk. Tumaini Gurumo, amesema sekta ya bahari ni muhimu kwakuwa asilimia 90 ya biashara yote duniani husafirishwa kwa njia ya maji.

“Ndani ya miaka mitatu tutaona mabadiliko makubwa, tutapata chuo ambacho kina mwonekano wenye hadhi ya kimataifa kama ambavyo kozi zetu zilivyo na hadhi ya kimataifa,” amesema Dk. Gurumo. 

Hata hivyo amesema hakuna uwiano mzuri baina ya wanafunzi wa kike na kiume kutokana na historia iliyojengeka kuwa sekta hiyo ni ya kiume zaidi.

“Tunaendelea kuwahamasisha wazazi ili waweze kuwaleta vijana wao hasa wa kike katika ubaharia. Kuna miongozo inayowalinda vijana wa kike wanaoingia katia sekta ya bahari hivyo wazazi wasiwe na hofu,” amesema.

Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Dk. Tumaini Gurumo, akionesha unga unaotumika kumwagwa baharini kama kiashiria kwa watumiaji wengine wa bahari pindi inapotokea ajali.

Mkuu huyo wa chuo amesema sekta ya bahari ina fursa nyingi na inaweza kuleta manufaa makubwa nchini ya kiuchumi na kuongeza ajira kwa vijana.

“Wanaoishi visiwani hawataweza kupata chakula kama hakitasafirishwa kutokea shambani kilipolimwa, lazima kipite kwenye vyombo vya majini.

“Tunafundisha wanaoviongoza, kuvijienga na kuvihudumia hivi vyombo, bila manahodha hatuwezi kuwa na meli au huduma ya meli haitakuwepo,” amesema Dk. Gurumo.

Amesema mwitikio wa wananchi katika maonesho ya Nanenane ni mkubwa kwani wamepata wageni wa rika mbalimbali ambao wamepewa mafunzo na kwamba wengi walikuwa hawafahamu kama kuna uhusiano wa shughuli zinazofanywa na chuo hicho na kilimo.

Amesema pia wanatekeleza dhana ya Uchumi wa Buluu kwa kuwapa wavuvi mafunzo ya usalama baharini na usalama kwenye maji.


Powered by Blogger.