SERIKALI YATATUA CHANGAMOTO MIGODI YA TANZANITE


Na Mwandishi Wetu Simanjiro

Serikali imeshughulikia changamoto za wachimbaji wadogo wa migodi ya Tanzanite zilizoathiri shughuli zao wakiwa migodini na kuhatarisha maisha yao.

Changamoto hizo ziliibuliwa wakati wa utekelezaji wa mradi wa Tanzanite kwa Uchumi Imara wa Mwanamke chini ya Chirika la Civic Social Protection (CSP) Manyara kwa ufadhili wa LSF.

Akizungumza Agosti 19, 2023 Kaimu Meneja wa Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, Izack Mgaya, amesema kulikuwa na ubovu wa barabara za kuelekea migodini, kutolewa mchanga kwa makundi ya kijamii yakiwemo wanawake na walemavu, uhaba wa vyoo na gharama za huduma hiyo kuwa juu pamoja na kutokuwa na huduma za kipolisi kikamilifu.

"Kupitia Shirika la CSP chini ya mradi wa Tanzanite kwa uchumi imara wa mwanamke unaofadhiliwa na LSF kuliibuliwa changamoto nyingi na ambazo zilitishia usalama wa maisha ya watu.

"Tulichukua changamoto za wachimbaji wa madini na kuzipeleka kamati ya ulinzi ya ukuta KUG, pia tulizifikisha uongozi wa ngazi ya juu pamoja na mkuu wa wilaya, mkurugenzi wa halmashauri na kwa Waziri wa Madini.

"Waziri Biteko alipofika hapa Mirerani alizitolea majibu.. hivi sasa mikakati mbalimbali imewekwa watu wa Tarura wameshakuja, mdau mkubwa wa madini na mchimbaji wa Kitalu C amekubali kushirikiana na Tarura kutengeneza barabara za migodini," amesema Mgaya

Amesema barabara zitakapokamilika zitarahisisha usafiri wa bodaboda ndani ya ukuta na bei zitapungua kutoka Sh 2,000 hadi 1000 na kwamba magari ya kutoa huduma za usafiri yataingia ndani ya ukuta wa Magufuli.

Eneo lingine ambalo kamati ya ukuta wanaendelea nalo ni gharama za huduma ya choo pamoja na mazingira kuwa machafu maeneo ya migodini.

"Suala la kijinsia liliibuka na tukashirikisha idara ya Polisi Mirerani ili wanawake wapate staha migodini, walifungua kituo kidogo ambacho kinafanya kazi na askari wameongezeka, vitendo vya unyanyasaji na upekuzi sasa ni tofauti na zamani wakati wa kutoka nje ya ukuta," amesema.

Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji
wa Shirika la CSP Manyara, Laizer Elihuruma, amesema lengo la mradi huo ni kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo kwa kuwa na miundombinu mizuri ikiwemo huduma za vyoo, upatikanaji wa haki ndani ya ukuta pamoja na kuwajengea wanawake uwezo wa kutatua changamoto za kijasiriamali.

"Kwa kushirijiana na Serikali tumeweza kupunguza baadhi ya changamoto zilizokuwa zinawakabili wanawake kupitia midahalo iliyohusisha viongozi wa Serikali, wakuu wa idara, dawati la jinsia na wasaidizi wa kisheria katika Mji mdogo wa Mirerani," amesema Laizer.

Amesema pia wameanzisha kituo cha msaada wa kisheria ambacho kinasimamiwa na wasaidizi wa kisheria ambao wanatoa elimu na msaada wa kisheria bure.

Akizungumzia changamoto za kisheria Msaidizi wa Kisheria, Nuru Mkireri, amesema awali kulikuwa na ukatili uliosababishwa na baadhi watu kutojua haki zao.

"Baadhi ya watu walivunjiwa haki zao bila kujua na hawakujua namna ya kutatua na kuzidai na kulazimika kuzipoteza jambo ambalo kwa kuwa na ofisi ya wasaidizi wa kisheria tumeendelea kutoa elimu na msaada wa kisheria ili kupunguza madhara," amesema Mkireri.

Amesema watu wengi wanazidi kuripoti matukio ya kihalifu ya Mirerani tofauti na awali kutokana na kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa jamii.
Powered by Blogger.