NELLY MSUYA KUONGOZA MWAUWASA


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemteua Nelly Msuya kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).

Kabla ya uteuzi huo Nelly alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Waziri Aweso pia ameunda timu ya wataalamu kutoka sekta ya maji watakaofanyia kazi changamoto ya huduma ya maji kwa wakazi wa Jiji la Mwanza sambamba na kusimamia kukamilika kwa mradi wa kuongeza maji katika mfumo wa usambazaji majisafi jijini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Maji, Florence Temba, timu hiyo itaongozwa na wataalamu kutoka Wizara ya Maji makao makuu.
Nelly Msuya akiwa na tuzo ya Afisa Mawasiliano Bora kutoka Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira aliyotunukiwa mwaka 2022.

Wataalam hao ni Mhandisi Mkama Bwire, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Mhandisi Charles Mafie, Mkurugenzi Msaidizi Uendeshaji na Matengenezo, Wizara ya Maji.

Wengine ni Mhandisi Nikas Mugisha Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma, Mhandisi Anthony Mayunga Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora, Mhandisi Valentine Njau Meneja wa Miradi ya Majisafi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (Dawasa) na Mhandisi Mwandamizi Ishmael Kakwezi, Mtaalamu wa Usimamizi wa Miradi.
Powered by Blogger.