MITI MILIONI 2.5 YAPANDWA KULINDA VYANZO VYA MAJI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma Zaidi ya miti milioni 2.5 imepandwa katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kulinda vyanzo vya maji.
Miti hiyo imepandwa kupitia kampeni ya upandaji miti rafiki wa maji iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango jijini Mbeya Novemba 2022.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameyasema hayo leo Agosti 16, 2023 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya utunzaji vyanzo vya maji, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Amesema miti 2,541,803 rafiki wa maji imepandwa sehemu mbalimbali nchini katika vyanzo vya maji na kwamba kampeni hiyo inaendelea ili kuhakikisha kila eneo lenye chanzo cha maji linawekewa mazingira rafiki ya kuliwezesha kutunza na kuzalisha rasilimali maji kwa uendelevu.
Kuhusu tathmini ya mazingira amesema Bodi za Maji za Mabonde sita kati ya tisa zimekamilisha tathimini ya kimkakati ya mazingira na Kijamii (SESA) ya Mipango shirikishi na mabonde saba yakikamilisha kazi ya mapitio ya mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya utunzaji vyanzo vya maji kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Eneo lingine lililofanyiwa kazi ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kunufaika na rasilimali maji ni kuanzishwa kwa kamati 17 za vidaka maji ambazo zinafanya kazi katika mabonde sita ya maji nchini.
Eneo lingine lililofanyiwa kazi ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kunufaika na rasilimali maji ni kuanzishwa kwa kamati 17 za vidaka maji ambazo zinafanya kazi katika mabonde sita ya maji nchini.
Aweso amefafanua kuwa kamati hizo zimekasimiwa baadhi ya majukumu ya Bodi za Maji ili kurahisisha usimamizi wa rasilimali maji katika eneo husika.
Amesema katika maeneo ya maji shirikishi Wizara ya Maji imeendelea kusimamia makubaliano ya kimataifa ili kuhakikisha ushirikiano huo unalindwa na kuifanya Tanzania kuwa salama katika matumizi ya maji.
Hatua hii imewezesha kujengwa kwa vituo nane vya kisasa vya kukusanya takwimu za mtiririko wa maji katika mito mikubwa ya Mara, Kagera, Simiyu na Rusumo iliyoko Bonde la Maji la Ziwa Victoria.
Waziri huyo amesema Wizara ya Maji imejifunza na kupata majawabu kupitia matukio mbalimbali ikiwemo tukio la ukame lililotokea miaka ya hivi karibuni na kusabisha baadhi ya mito kuwa na upungufu wa maji.
“Hatutaki na hatutegemei haya yajirudie tena siku nyingine," amesema Aweso.
Wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Wizara ya Maji kwa utayari wake wa kuhakikisha maagizo mbalimbali yanayotolewa na viongozi yanatekelezwa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jackson Kiswaga, ameitaka wizara ihakikishe inaendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo ya viongozi kwani maji ni rasilimali muhimu ambayo haina mbadala.

