KILO BILIONI 2 ZAUZWA KWA STAKABADHI GHALANI
Na Nora Damian, Mbeya
Zaidi ya kilo bilioni 2.2 za mazao mbalimbali zimeuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani tangu ulipoanza kutumika 2017/18 huku korosho ikiongoza kwa asilimia 89.
Akizungumza Agosti 4, 2023 kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya Meneja Mipango na Uhamasishaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani, Sura Ngatuni, amesema kupitia mfumo huo bei za mazao zimeimarika.
Ametolea mfano wa kokoa ambayo imeongezeka kutoka Sh 5,000 kwa kilo mwaka 2022 na kufikia Sh 7,525 wakati ufuta umeongezeka kutoka Sh 3,100 na kufikia Sh 4,105.
“Tumetoa elimu na wakulima wengi wameshaelewa maana ya mfumo, pia ubora wa mazao nao umechangia wa wanunuzi kupata mazao sehemu moja na kwa kiasi kizuri…mazao yanapitia katika mfumo yana ubora mzuri, yamepimwa kwa kutumia kilo na mnunuzi anaamini hataibiwa,” amesema Ngatuni.
Amesema pia wameongeza mazao mapya katika mfumo huo ya vitunguu swaumu na mbaazi yanayolimwa Mkoa wa Manyara baada ya kuhamasisha wananchi.
Amewashauri wakulima waendelee kujifunza kuhusu mfumo huo ili waweze kuuza mazao kupitia stakabadhi za ghala na kuepuka kuyumbishwa na wafanyabiashara wachache.
Naye Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dk. Benson Ndiege, amesema mfumo wa stakabadhi ghalani umeleta ufanisi mkubwa.
“Mfumo unawasaidia wakulima wanakuwa na sauti moja kwa sababu usipokuwepo mnunuzi anakwenda kumtafuta mkulima mmoja mmoja na inakuwa ni rahisi kumlaghai,” amesema Dk. Ndiege.
Amesema pia kupitia mfumo huo ni rahisi mkulima kupata taarifa za soko, kupata mazao bora, kuwa na takwimu sahihi za mauzo na mapato.

