BILIONI 147 ZALIPWA WAKULIMA WA KOROSHO MAMCU


Ofisa Kilimo wa Chama Kikuu cha Ushirika Masasi Mtwara, Martha Shirima, akionesha mashine ya kupima unyevu wa korosho katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya
.

Na Nora Damian, Mbeya

Chama Kikuu cha Ushirika Masasi Mtwara (MAMCU LTD) kimelipa zaidi ya Sh bilioni 147.7 kwa wakulima wa korosho katika msimu wa mwaka 2021/22.

Chama hicho kinahudumia Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Mtwara Manispaa, Nanyamba, Masasi Mjini, Masasi Wilaya na Nanyumbu ambako kuna jumla ya vyama 192.

Akizungumza Agosti 6, 2023 katika Kijiji cha Ushirika kilichopo kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, Ofisa Kilimo wa chama hicho, Martha Shirima, amesema fedha hizo zimelipwa kupitia vyama vyao vya msingi.

“Kuna changamoto za wakulima kutaka fedha kwa haraka na wakati mwingine kuuza mazao kabla ya kuyaleta kwenye chama, tunaendelea kufanya maboresho ili kumfanya mkulima asiwe na haraka ya kuuza mazao yake kwa mtu mwingine.

“Wakiuza kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani wanapata faida nyingi, tunawadhamini, wanapata vifungashio, tunasimamia malipo wanayapata kihalali, tunawapa mafunzo kupitia maofisa kilimo, tunawapa miche ya korosho bure na tunawasaidia kupata pembejeo bure,” amesema Shirima.

Kuhusu uzalishaji wa korosho kwa mwaka 2022/23 amesema wameuza kilo 59,607,667 kwa thamani ya Sh 111,449,764,229 kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo bei ya juu ilikuwa Sh 2,200 na ya chini Sh 1,700.


Ofisa Kilimo wa Chama Kikuu cha Ushirika Masasi Mtwara, Martha Shirima, akionesha korosho zinazozalishwa na wanachama wa MAMCU katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Amesema pia chama kimefanikiwa kudhibiti ubora wa korosho kwa kununua vipima unyevu 175 na mizani na kuvigawa kwa wakulima ili kuwawezesha kujua unyevu wa korosho kabla ya kupelekwa kuhifadhiwa kwenye maghala makubwa.

Amesema pia chama kimenunua hekari 1500 wa ajili ya kilimo cha ufuta na mikorosho itakayotumika kama mashamba darasa.

Mbali ya korosho chama hicho pia kinahudumia mazao ya ufuta na mbaazi ambapo kwa msimu wa mwaka 2023 kimeuza kilo 17,111,270 za ufuta kwa thamani ya Sh 61,261,338,927 ambapo bei ya juu ilikuwa Sh 3,967 kwa kilo na ya chini Sh 3,560.

Ofisa huyo amesema pia chama kilinunua mbegu za ufuta tani 10 zenye thamani ya Sh milioni 65 na kuzigawa kwa wakulima ili kuhakikisha wanapata bei nzuri kwa kuzalisha ufuta mweupe.

“Mbaazi ni zao ambalo tumeliongeza kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu chama kimekua na tunatarajia mwezi huu (Agosti 11) ndiyo itakuwa mnada wetu wa kwanza. Itatusaidia kujua uzalishaji ni kiasi gani na namna ambavyo wakulima watanufaika,” amesema Shirima.

Chama hicho kimefanikiwa kujenga maghala makuu matatu katika Wilaya za Mtwara, Masasi na Nanyumbu ili kusogeza huduma karibu za kuhifadhi mazao kabla ya kupiga mnada.



Powered by Blogger.