KIGAHE AHAMASISHA WAKULIMA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe (kushoto), akipata maelezo baada ya kutembelea banda la Wakala wa Vipimo katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya. Katikati ni Mkurugenzi wa Huduma za Biashara WMA, Deogratias Maneno.
Na Nora Damian, Mbeya
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amewataka wakulima kujiunga kwenye vikundi na vyama vya ushirika ili kuwa na mizani
Amesema bado kuna changamoto za vipimo visivyo sahihi kama vile lumbesa, kangomba, majaba, butura na nyingine na kushauri Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuendelea kutoa elimu kwa wakulima.
Akizungumza Agosti 5, 2023 baada ya kutembelea banda la WMA kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya amesema wakulima wakielewa umuhimu wa vipimo sahihi watahamasika kuvitumia.
“Wakulima wasikubali kuuza mashambani kwa sababu kule huwezi kupima, wakielewa umuhimu wa vipimo watahamasika kuungana na kununua mizani,” amesema Kigahe.
Maofisa wa Wakala wa Vipimo wakitoa elimu kwa wananchi waliotenbelea banda lao katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Ameutaka wakala huo kwenda maeneo mbalimbali ya nchi na kuwaelimisha wakulima umuhimu wa kutumia vipimo sahihi na kujiunga katika vikundi au ushirika ili iwe rahisi kupata bei nzuri ya mazao yao.
Ameutaka wakala huo kwenda maeneo mbalimbali ya nchi na kuwaelimisha wakulima umuhimu wa kutumia vipimo sahihi na kujiunga katika vikundi au ushirika ili iwe rahisi kupata bei nzuri ya mazao yao.
“Kwa mkulima mmoja mmoja si rahisi kuwa na mzani, lakini kwa umoja wao wanaweza kuwa na mizani ambayo itawasaidia kuuza mazao yao kwa vipimo. Tunaamini wakiwa kwenye vikundi, vyama vya ushirika hata Serikali itakuwa rahisi kutoa huduma,” amesema Kigahe.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Biashara WMA, Deogratias Maneno, amesema wanahamasisha upimaji mazao na bidhaa mbalimbali kwa kutumia mizani kwa kuwa ndio suluhisho la kuondokana na vipimo visivyo sahihi.
Amesema kwa sasa mizani ipo ya kutosha wakulima wanaweza kujiunga kwenye vikundi na kuweza kununua.
Aidha amesema wameweka utararibu katika mazao ya kimkakati kama vile pamba na korosho kwa kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi na kuepuka kuuza mazao kiholela.

