VETA YAONESHA UBUNIFU MTAMBO MAZIWA YA UNGA
Mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta - Dar es Salaam, Emmanuel Bukuku, akionesha
mtambo alioubuni wa kuyaongezea maziwa thamani katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Na Nora Damian, Mbeya
Kilio cha wafugaji kukosa masoko ya uhakika ya maziwa huenda kikawa historia baada ya Chuo cha Ufundi Stadi Veta kutengeneza mtambo wa kuyaongezea thamani.
Aliyebuni mtambo huo ni Mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta - Dar es Salaam, Emmanuel Bukuku.
Akizungumza Agosti 6, 2023 katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutengeneza maziwa ya unga kutoka maziwa ya maji.
“Niligundua wafugaji wengi wanapeleka maziwa kwenye vyama vya ushirika lakini wakati mwingine vyama vinashindwa kuyanunua yote na mengine huharibika.
“Tuliona yakiongezewa thamani na kuwa katika mfumo wa unga yanaweza kusafiri kirahisi ndiyo maana tulibuni mashine hii,” amesema Bukuku.
Mwalimu huyo amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutengeneza lita nane za maziwa ya maji na kupata kilo moja ya maziwa ya unga kwa dakika nane mpaka 10.
Amesema mashine hiyo inafanya kazi vizuri kwani tayari wameifanyia majaribio ambapo wanatarajia kuipeleka kwenye maeneo ambayo maziwa yanapatikana kwa wingi.
“Mikoa ambayo tunaona mashine hii inaweza kufanya kazi vizuri mfugaji akapata faida ni Mbeya eneo la Tukuyu ambapo lita moja ya maziwa inauzwa kati ya Sh 500 mpaka Sh 1,000 na maeneo ya Njombe na Shinyanga,” amesema.
Amesema mashine hiyo yenye thamani ya Sh milioni 6 ina uwezo wa kuchakata mapipa mawili ya maziwa kwa siku moja.
Amesema kwa viwanda vikubwa wakipata wateja wanaweza kutengeneza mashine kubwa zaidi ya hiyo.
“Wafugaji wakitumia mashine hii watapata faida kubwa na inaweza kuwekwa kwenye vituo vya kukusanya maziwa. Maziwa ya maji yanauzwa wastani wa Sh 1,100 kwa lita lakini kilo moja ya maziwa ya unga inauzwa Sh 18,000,” amesema Bukuku.
