EWURA YAHAMASISHA UJENZI VITUO VYA MAFUTA VIJIJINI



Ofisa Uhusiano wa Ewura, Tobietha Makafu, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.


Na Nora Damian

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imewataka wadau mbalimbali kuchangamkia fursa ya kujenga vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini ili kusogeza huduma hiyo pembezoni.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 2, 2023 kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Ofisa Uhusiano wa Ewura, Tobietha Makafu, amesema lengo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma katika maeneo husika.

Amesema wamerahisisha masharti ya gharama za vibali na leseni ambazo ni nafuu kulinganisha na za ujenzi wa vituo vya mafuta mjini ili nishati hiyo iweze kupatikana kirahisi maeneo mengi.

“Shughuli za uzalishaji zimeongezeka mpaka vijijini, tunaamini watu wanahitaji mafuta ya kutosha, kwa kijijini unaweza kuwa na tanki la mafuta la kuanzia lita 4,500 mpaka 5,000, kiwanja kuanzia mita za mraba 400 na pampu moja.

“Kama una mtaji wa kati ya shilingi milioni 40 mpaka 60 unataka kujenga kituo cha gharama nafuu vijijini tutakueleza taratibu za kufuata upate kibali cha ujenzi na leseni,” amesema Tobietha.



Wananchi wakipata maelezo kutoka kwa maofisa wa Ewura walipotembelea banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika viwanja vya John Mwakangale, jijiji Mbeya.

Amezitaja gharama hizo kuwa ni kibali cha ujenzi (Sh 50,000), maombi ya leseni ya biashara (Sh 50,000) na kufanya biashara ya kituo cha mafuta (Sh 100,000).

Katika maonesho hayo mamlaka hiyo pia inatoa elimu ya udhibiti wa huduma za nishati na maji petroli yaani umeme, gesi asilia, sekta nzima ya maji na usafi wa mazingira.

Aidha wanahamasisha uwekezaji katika miradi ya petroli na gesi hasa kwa watu wanaotaka kutoa huduma katika ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Ohima - Uganda hadi Chongoleani Tanga na kusisitiza lazima wasajiliwe katika kanzidata ya Ewura.

“Tunatoa elimu kwa wakulima kwa sababu tunaamini ni watumiaji mkubwa wa umeme, maji na nishati ya petroli, tunawaelimisha namna wanavyoweza kupata haki zao za msingi katika matumizi ya huduma hizi.

“Kama kuna mtu ana malalamiko na mtoa huduma wa nishati ya umeme au maji, amemlalamikia hajapata suluhisho afike ili aweze kupata haki zake za msingi,” amesema.



Powered by Blogger.