AMO KUWEZESHA VIJANA 50 KUJIKWAMUA KIUCHUMI
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akitoa mada wakati wa kongamano la vijana lililoandaliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Amo, Dar es Salaam.
Na Nora Damian, Dar es Salaam
Vijana wajasiriamali 50 wanatarajia kupatiwa vitendea kazi mbalimbali ili waweze kukuza shughuli zao na kujikwamua kiuchumi.
Vitendea kazi hivyo kama vile bodaboda, vyerehani, vifaa vya saluni, majiko ya gesi vitatolewa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la AMO linalojihusisha na uwezeshaji vijana, wanawake, watoto na watu wenye uhitaji maalumu.
Akizungumza Agosti 12, 2023 wakati wa kongamano la vijana lililokwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Amina Said, amesema wanalenga kumuamsha kijana kujitambua na kujua thamani yake kwani asipojielewa na kujithamini ni vigumu kufanikiwa.
“Tunatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ndiyo maana tumeweka mikakati ya kuwezesha kundi hili kwa lengo la kutatua changamoto za ajira zinazolikabili.
“Amo inamuamsha kijana aweze kujiongoza mwenyewe na kutimiza malengo yake binafsi,” amesema Amina.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AMO, Amina Said, akizungumza wakati wa kongamano lililoshirikisha vijana wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, ambaye alikuwa mgeni rasmi amewataka vijana kujituma kufanya kazi kwa bidii na kuacha kuchagua kazi ili wajikwamue kiuchumi.
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, ambaye alikuwa mgeni rasmi amewataka vijana kujituma kufanya kazi kwa bidii na kuacha kuchagua kazi ili wajikwamue kiuchumi.
Amesema Serikali inathamini vijana ndio maana inatekeleza program mbalimbali ikiwemo ya BBT (Jenga Kesho Iliyo Bora) na nyingine kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi.
“Hiki ni kipindi cha watu kufanya kazi, kuwa na masters, degree haimaanishi huwezi kuwa mama lishe. Watu wengi wamefanikiwa kwenye kilimo kwahiyo elimu sio kigezo cha kutolima au kufanya kazi nyingine za mikono,” amesema Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala.
Pia amewaasa vijana kujiepusha na maadili mabaya na kuheshimu mila na desturi za Kiafrika.
“Mjiepushe na ‘Ilove you’, kuna baadhi ya wanaume waongo, kwa siku atawaambia wanawake saba ‘Ilove you’ ili apate anachokitaka na akitoka hapo anakutangaza…achaneni na mambo hayo akitaka kugusa mwili wako mwambie ‘don’t touch me’,” amesema.
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, akizungumza wakati wa kongamano la vijana lililoandaliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la AMO na kufanyika Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambaye alitoa mada kuhusu umuhimu wa vijana kuwa wawajibikaji, Edward Mpogolo, amewataka vijana kuacha na tamaa na badala yake wawe na nidhamu kwenye maeneo yao ya uwajibikaji.
“Unakuta mtu hajawajibika vizuri kwenye nafasi ya afisa tarafa halafu anatamani ukuu wa wilaya, kosa letu vijana wengi ni tamaa.
“Usipokuwa na nidhamu kwenye eneo la uwajibikaji utajikuta unaingia gharama zisizokuwa na manufaa,” amesema Mpogolo.
Mkufunzi wa masuala ya vijana, Rodrick Nabe, amesema vijana wasipofanya juhudi watapoteza ndoto zao.
Katika kongamano hilo vijana wamejifunza mambo mbalimbali kama vile kujitambua, masuala ya biashara na uwekezaji, masoko, na fursa zinazopatikana nchini.


