TANZANIA, MALAWI KUZALISHA MEGAWATI 180 ZA UMEME
Waziri wa Nishati, January Makamba (kulia) na Waziri wa Nishati, Ibrahim Matola, wakionesha hati za makubaliano ya ushirikiano wa kuzalisha umeme kupitia Mto Songwe.
Na Nora Damian, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania na Malawi zimekubaliana kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya Maji ya Mto Songwe pamoja na kuendeleza rasilimali za mto huo.
Akizungumza Agosti 11, 2023 wakati wa kusaini makubaliano hayo Dar es Salaam, Waziri wa Nishati, January Makamba, amesema wanatarajia kuzalisha umeme wa megawati 180 kwa kutumia maporomoko ya Mto Songwe.
Amesema makubaliano hayo yanafuatia maelekezo ya marais wa nchi hizo, Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Lazarus Chakwera walipokutana hivi karibuni ambapobwalikubaliana kuendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali kudumisha uhusiano uliopo.
Amesema makubaliano hayo pia yatahusisha ujenzi wa miundombinu ya umeme na katika eneo la gesi ambapo Tanzania inatarajia kuuza gesi Malawi.
"Kutakuwa na kamati ya pamoja ya mawaziri na kamati ya wataalam ambapo kila upande utateua wataalam na vikao vitaanza rasmi Oktoba mwaka huu.
"Kutokana na maelekezo ya viongozi wetu Rais Samia Suluhu na Rais Chakwera walikubaliana tuongeze maeneo ya ushirikiano hasa eneo la nishati," amesema Makamba.
Aidha amesema hiyo ni sehemu ya mradi wa kikanda wa kuwa na gridi moja katika kanda hii.
"Tunaamini miradi hii itanufaisha nchi zetu kwa sababu mahitaji ya umeme bado ni makubwa, ushirikiano huu utaimarisha uhusiano kati ya nchi zetu," amesema.
Waziri Makamba amesema pia upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga njia ya kusafirisha umeme itakayounganisha nchi hizo tayari umekamilika na sasa wanatafuta fedha uanze kutekelezwa.
Amesema kamati ya wataalam itaamua eneo sahihi la mradi kutokana na taarifa za kiufundi zitakazopatikana.
Naye Waziri wa Nishati Malawi, Ibrahim Matola, amesema makubaliano hayo yataleta manufaa kwa nchi zote mbili.
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, akizungumza baada ya ujumbe wa Serikali ya Malawi kutembelea Kituo cha Kuchakata Gesi Asilia cha Kinyerezi 1. Watatu kushoto ni Waziri wa Nishati Malawi, Ibrahim Matola.
Amesema nchi nyingi Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki bado hazina nishati ya kutosha hivyo ni muhimu kuwe na miradi mingi zaidi katika sekta hiyo.
"Rais Samia na Rais Chakwera walikubaliana kushirikiana pamoja kwa manufaa ya mataifa haya. Makubaliano haya ni mwanzo wa safari yetu ya kushirikiana katika nyanja nyingi," amesema Matola.


