MALENGO YA CRDB MARATHON 2023 YAMETIMIA

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi (Wanne kushoto), akipokea mfano wa hundi ya Sh milioni 100 zilizokabidhiwa na Benki ya Crdb kwa Wizara ya Afya Zanzibar kujenga kituo cha afya cha mama na mtoto. Watatu kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Crdb, Abdulmajid Nsekela.

Na Nora Damian, Dar es Salaam

Benki ya CRDB imefanikiwa kukusanya fedha kwa ajili ya kuboresha afya ya mama na mtoto ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya Zanzibar kupitia mbio za hisani ‘Crdb Marathon’.

Mbio hizo zimefanyika leo Agosti 13, 2023 katika viwanja vya The Green Oysterbay, Dar es Salaam na kushirikisha washiriki zaidi ya 7,000 kutoka ndani nan je ya nchi waliokimbia kilomita 5, 10, 42 pamoja na waendesha baiskeli.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye alikuwa mgeni rasmi ameipongeza benki hiyo kwa ubunifu na kujitoa kusaidia jamii na kuomba siku zijazo Zanzibar iwe mwenyeji.

“Nawapongeza Crdb kwa ubunifu wenu na kujitoa, huduma ya afya ya mama na mtoto ni moja ya eneo lililopewa kipaumbele na serikali zote mbili. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya jitihada kubwa za kuimarisha huduma za afya na kujenga miundombinu mipya,” amesema Rais Mwinyi.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi (katikati), akiwa na wakimbiaji wengine wakishiriki mbio za hisani za Crdb Marathon, Dar es Salaam.

Mbio hizo zenye kaulimbiu ya ‘Kasi isambazayo tabasamu’ zimefanyika kwa mara ya nne tangu zilipoanza mwaka 2020.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema zinalenga kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto na kuboresha utunzaji mazingira.

Kwa mujibu wa Nsekela, tangu mbio hizo zianze zimewezesha upasuaji wa watoto zaidi ya 300 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ujenzi wa kituo cha mawasiliano katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kinamama wenye ujauzito hatarishi na changamoto ya fistula katika Hospitali ya CCBRT.
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akipokea mfano ya hundi ya Sh milioni 20 ilizokabidhiwa na Benki ya Crdb kwa Baraza la Manispaa ya Mji Mkoa wa Mjini Magharibi kuboresha bustani.

Amesema mwaka 2020 zilishirikisha washiriki zaidi ya 4,000 na kufanikiwa kukusanya Sh milioni 200, mwaka 2021 washiriki zaidi ya 5,000 na kukusanya Sh milioni 350, mwaka 2022 washiriki zaidi ya 6,000 na kiasi kilichokusanywa ni Sh milioni 470.

Amesema mwaka huu mbio hizo zimeshirikisha zaidi ya washiriki 7,000 kutoka ndani na nje ya nchi.

Mbali ya kusaidia ujenzi wa kituo cha afya ya mama na mtoto Zanzibar pia fedha zitakazopatikana zitasaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo katika Hospitali ya Jakaya Kikwete na kinamama wenye ujauzito hatarishi na changamoto ya fistula katika Hospitalio ya CCBRT.

Aidha kupitia kampeni yake ya Pendezesha Tanzania benki hiyo itaboresha bustani za Zanzibar ambazo ni bustani ya Jamhuri, Migombani, Tenga Mnazi Mmoja, mbele ya Ikulu na njia nne za Michenzani.

“Mbio hizi zitakuwa endelevu wa masilahi mapana ya jamii na nchi yetu,” amesema Nsekela.

Benki hiyo pia inatarajia kuanza mbio maalumu zitakazofanyika wakati wa Tamasha la Kizimkazi Zanzibar ambazo zitaenda sambamba na utoaji wa boti mpya kwa washiriki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Crdb, Abdulmajid Nsekela, akivalishwa nishani na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, baada ya kumaliza mbio za hisani zilizoandaliwa na benki hiyo. Kulia ni Mke wa Rais Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi.

Aidha itajega soko la kisasa la samaki kuunga mkono juhudi za Rais Mwinyi za kuendeleza dhana ya Uchumi wa Buluu.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Bima ya Sanlam ambao ndio wadhamini wakuu, Julius Magabe, amesema wanajivunia kuwa sehemu ya mbio hizo ambapo wamekuwa wakiongeza udhamini kila mwaka kutokana na matunda wanayoyaona.



Powered by Blogger.