WABUNGE, MADIWANI KUPIMWA KWA KAZI

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abas Mtemvu, akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kinyerezi, Dar es Salaam.
Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, akizungumza katika mkutano wa hadhara kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi uliofanyika katika jimbo hilo.

Na Nora Damian
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimesema kitawashughulikia wabunge na madiwani wasioshiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwenye maeneo yao.

Mara kadhaa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abas Mtemvu, kupitia vikao vyake mbalimbali amekuwa akisisitiza wenyeviti wa Serikali za Mitaa, madiwani na wabunge kushiriki kikamilifu katika utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Mtemvu ameeleza hayo jijini Dar es Salaam leo Julai 23,2023 katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi uliofanyika katika jimbo hilo. 

“Mbunge au diwani kama kwako hujafanya kazi hutufai, Dar es Salaam tutapimana kwa uwezo wa kazi. Siasa ni maisha, unapochagua kiongozi chagua ujue anakuja kukutumikia…huyu mama (Bonnah Kamoli) tayari ana vituo sita na kata ambazo hazina tutajenga.

“Wengine wananuna, wale wenye maneno watuache tufanye kazi, tumalize kata zote halafu tutarudi kwenye matawi na mitaa…wenyeviti wapigaji wasitarajie tena kupata nafasi,” amesema Mtemvu.

Naye Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amesema katika kipindi cha 2015/2020 jimbo hilo lilikuwa halina miundombinu mizuri lakini kwa miaka miwili wametekeleza miradi yenye thamani ya Sh bilioni 28.

“Segerea ni jimbo la nane kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, shule za sekondari zilikuwa na mazingira mabovu lakini tunaishukuru Serikali kwa mambo makubwa iliyotufanyia,” amesema Bonnah.

Ameitaja baadhi ya miradi inayoendelea kwenye jimbo hilo kuwa ni ujenzi wa vituo vya afya katika Kata za Kinyerezi, Segerea na Mnyamani.

Kwa upande wa barabara ni ile ya Bonyokwa – Segerea (kilomita 3.2), Kisukuru – Bonyokwa na Majichumvi.

Kwa mujibu wa Bonnah miradi mingine itatekelezwa kupitia Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwa upande wake Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde, ambaye alikuwa mgeni mwalikwa katika mkutano huo amewataka Watanzania kutumia majukwaa sahihi kuishauri Serikali kuhusu suala la uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

“Tuishi kwa kuvumiliana ili tusije tukavuruga amani ya nchi yetu, tukae kwa kutulia tukijua mama (Rais Samia) hawezi kutuangusha…tubishane naye kwa hoja,” amesema Lusinde.

Powered by Blogger.