'ELIMU YA JUU ELEKEZENI TAFITI MPANGO WA MAENDELEO'
Na Nora Damian
Taasisi za elimu ya juu zimetakiwa kuelekeza tafiti na bunifu zao katika maeneo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo wa maendeleo wa miaka mitano (2021/22 – 2025/26).
Mpango huo unasisitiza na kuhimiza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu hasa matumizi ya takwimu, mitambo inayojiendesha, kompyuta na robot.
Akizungumza Dar es Salaam Julai 22,2023 wakati wa kufunga maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga, amesema maendeleo makubwa na ya haraka ya sayansi na teknolojia yamesababisha kuwapo kwa ubunifu wa teknolojia mpya yakilenga kurahisisha maisha.
“Taasisi za elimu ya juu zijikite katika matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kutimiza azma ya Serikali katika Mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano,” amesema Kipanga.
Naibu Waziri huyo pia amezitaka taasisi zilizoshiriki maonesho hayo kujipambanua na kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya mwaka huu inayosisitiza ‘Kukuza ujuzi nchini kupitia elimu ya juu, sayansi na teknolojia kwa uchumi imara na shindani’.
“Taasisi za elimu ya juu zina mchango mkubwa katika kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kuhakikisha wahitimu wetu wanapata ujuzi na maarifa stahiki na shindani katika soko la ajira na wanashiriki kikamilifu kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema.
Aidha amesema Serikali itaendelea kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu nchini kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Kipanga, wizara ilitoa mafunzo kwa wabunifu wachanga 83 na kutoa rasilimali fedha kwa wabunifu 27 walioibuliwa katika mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ya mwaka 2022.
Maonesho hayo yaliyoratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yameshirikisha taasisi 85 kutoka ndani na nje ya nchi ambapo zimeongezeka kutoka taasisi 75 za mwaka jana.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amesema kati ya taasisi hizo 77 ni za ndani.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga (katikati), akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Udahili na Menejimenti ya Data Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Dk. Kokuberwa Katunzi alipotembelea banda la TCU wakati wa kufunga Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyomalizika Julai 22, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa.

