AKILI BANDIA YAUNDIWA MKAKATI UDOM
Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Lugano Kusiluka, akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakiwahudumia wananchi waliofika kwenye banda lao kupata maelezo ya programu na taratibu za udahili kwa mwaka wa masomo 2023/2024.
Na Nora Damian
Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimewataka Watanzania kujiandaa kuanza kuitumia Teknolojia ya Akili Bandia (ChatGPT) badala ya kuihofia.
Tangu kuzinduliwa kwake mwishoni mwa Novemba 2022, ChatGPT inayotumia akili bandia kujibu maswali au kuunda ujumbe unapohitajika kutoka kwa watumiaji, imekuwa programu ya intaneti inayokua kwa kasi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 17,2023 kwenye maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Lugano Kusiluka, amesema wameanza kutoa kozi fupi kuhusu teknolojia hiyo.
"Artificial Inteligence (akili bandia) imefika mahali inaanza kutuchanganya, Udom tunao wataalam wameanza kutoa kozi fupi ili Watanzania wajitayarishe kuitumia kwa sababu imetukuta hatuwezi kuikimbia," amesema Profesa Kusiluka.
Teknolojia hiyo imesababisha mapinduzi ya rasilimali watu ambapo Kampuni kubwa ya kiteknolojia IBM imetangaza kuacha kuajiri watu ili kushughulikia takriban kazi 8,000 ambazo zinaweza kusimamiwa na akili bandia.
Chuo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 30,000 kina programu za shahada za awali zaidi ya 80, uzamili na uzamivu.
Profesa Kusiluka amesema fani zote zinazofundishwa nchini zinapatikana katika chuo hicho.
Amesema pia chuo hicho kinafanya vizuri katika maeneo mbalimbali hasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambapo wamekuwa washindi katika mashindano yanayofanyika ndani na nje ya nchi.
"Tunawaandaa vijana wetu kujiajiri, tunajua fursa za ajira si nyingi lakini zipo kama na wewe unayesoma unajihesabu ni mmojawapo wa watu wanaoweza kutengeneza fursa za ajira yako mwenyewe na kuajiri watu wengine.
"Pamoja na taaluma tunafundisha ujasiriamali kwa kuamini kwamba anayepata fursa ya kuja chuo kikuu amewaacha wengine wengi ambao hawajapata fursa ili akirudi washirikiane," amesema.
Amesema katika maonesho hayo wanawaelimisha wanaotaka kujiunga na chuo namna ya kuingia kwenye mifumo ya kujisajili na kuchagua programu wanazohitaji, taarifa kuhusu tafiti mbalimbali, machapisho na maendeleo ya teknolojia.

