SERENGETI WATAKA MAJI KUTOKA ZIWA VICTORIA
Na Mwandishi Wetu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja amewaagiza wataalam wa Wizara wa Maji kufanya utafiti kujua namna bora ya kuwezesha upatikanaji endelevu wa huduma ya maji kwa wananchi wa Serengeti.
Ametoa taarifa hiyo baada ya kupokea maelezo ya Mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Amsabi Mrimi, kuwa kina cha maji kimepungua kwenye Bwawa la Manchira ambalo ni chanzo cha maji cha mradi wa maji wa Mugumu unaotarajiwa kuhudumia wakazi wa eneo hilo.
Luhemeja amesema utekekezaji wa mradi huo unaruhusu kusanifu na kujenga hivyo wataalam waje na ushauri iwapo kuna umuhimu wa mradi huo kutumia maji ya Ziwa Victoria kupitia mradi wa Tarime - Rorya ambao utekelezaji wake unaendelea.
"Katika Wilaya ya Serengeti wananchi wanatumia maji kutoka Bwawa la Manchira kama chanzo cha maji, lakini mheshimiwa Mbunge anaonesha wasiwasi kwamba inawezekana bwawa hili lisiwe chanzo endelevu kutoa huduma katika eneo hili kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri ujazo wa maji," amesema Luhemeja.
Mhandisi Luhemeja ametoa wito kwa wananchi wa Serengeti kutunza vyanzo vya maji ili kupunguza athari zinazoweza kukumba vyanzo hivyo.Aidha Dkt. Amsabi ameishukuru Serikali kwa kutenga Sh bilioni 20 kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Serengeti.
"Ongezeko la watu katika mji huu ni kubwa, utalii unakua kwa kasi na maji yanahitajika, chanzo tulichonacho kwa sasa Bwawa la Manchira limezidi kupungua maji kutoka mita tisa mpaka sita tangu lilipotengenezwa, ni muhimu wananchi wapate maji kutoka Ziwa Victoria ambacho ni chanzo cha uhakika," amesema Mrimi.
Kaimu Ofisa Maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Wiston Agwaro, amesema chanzo cha maji cha Bwawa la Manchira kinatosheleza kwa mahitaji ya sasa.
Amekiri kuwepo na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha kupungua kwa maji.

