UDOM WAJIPAMBANUA MIRADI YA MAENDELEO

Na Nora Damian
Chuo Kikuu cha Dodoma kimesema kitaendelea kutoa ushauri wa kitaalam kuhakikisha malengo ya mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) yanafikiwa. 

Mradi huo ambao ni maalumu kwa vijana ulizinduliwa Machi,2023 ambapo vijana 812 walichaguliwa kujiunga. 

Programu hiyo ya BBT ambayo ipo katika hatua za mwisho inaendelea katika vituo 13 nchini na baada ya kukamilika vijana watapelekwa shambani kuanza uzalishaji wa mazao kwa vitendo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Julai 22,2023 kwenye maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson, amesema lengo ni kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha miradi ya maendeleo. 

“Tumeshiriki kikamilifu katika mradi huu na tupo tayari kuendelea kushiriki, Chuo kikuu cha Dodoma kinajipambanua na kinaweza kushirikiana na Watanzania kutoa ushauri wa namna bora ya kushiriki katika kilimo kama BBT na miradi mingine ambayo Serikali imejikita kuitekeleza,” amesema Profesa Wineaster.

Amesema pia chuo hicho kinazalisha maarifa mbalimbali pamoja na kufanya tafiti na kuibua bunifu kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Chuo hicho kimetumia maonesho hayo kuelimisha umma kuhusu program mbalimbali ilizonazo ikiwemo teknolojia ya Akili Bandia (Artificial Inteligence) ambayo itaanza kufundishwa chuoni hapo.

Udom chenye wanafunzi zaidi ya 32,000 kinafundisha fani zote zinazopatikana nchini ambapo pamoja na taaluma kinafundisha ujasiriamali kwa kuwaandaa vijana kujiajiri na jkuajiri watu wengine. 
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wineaster Anderson, akiangalia machapisho mbalimbali ya chuo hicho kwenye maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Dar es Salaam

Powered by Blogger.