MRADI WA MAJI SENGA KUKAMILIKA 2025
Na Mwandishi Wetu, Geita
Mradi wa maji wa miji 28 - Senga wilayani Geita unaotarajiwa kuhudumia vijiji 19 na kata 13 utakamilika Oktoba 2025.
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya AFCON na kusimamiwa na Mkandarasi mshauri WAPCOS.
Akizungumzia mradi huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amemtaka mkandarasi kufanya kazi kwa saa 24 ili kuukamilisha ndani ya muda husika.
"Mkoa wa Geita unakua kwa kasi , uwepo wa migodi na ongezeko la watu limesababisha mahitaji makubwa ya maji wakati uhalisia upatikanaji wa maji kimkoa ni chini ya asilimia 50 kitu ambacho si sawa," amesema Luhemeja.
Amewataka wasimamizi wa mradi wahakikishe wanamsimamia mkandarasi ili utekelezaji wake uwe katika kiwango cha kutosheleze mahitaji ya Mji wa Geita na maeneo yote yanayotarajiwa kuhudumiwa kwa muda mrefu.
Mhandisi Luhemeja amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maji ambayo inaendelea maeneo mengi ya nchi.
"Fedha za mradi zipo, vifaa vipo, mkandarasi asimamiwe kufanya kazi kwa kasi ili mradi ukamilike wananchi wa Geita wapate huduma endelevu ya majisafi, hakutakuwa na muda wa nyongeza," amesema Luhemeja.
Mradi wa maji wa miji 28 - Senga unagharimu Sh bilioni 128 na chanzo cha maji yake ni Ziwa Victoria.

