UPASUAJI MTOTO WA JICHO WAOKOA 25 KITETO


Muuguzi Mkuu wa Kituo cha Afya Anglikana Kiteto,  Saraweki Mbelwa, akimhudumia mmoja wa wananchi wa Kiteto aliyejitokeza kupatiwa huduma za mcho.


Na Mwandishi Wetu, Kiteto

Wakazi 25 wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kwa ushirikiano wa Kituo cha Afya Anglikana Kiteto na Hospitali ya Mvumi Dodoma.

Akizungumza Julai 28,2023 wakati wa utoaji huduma hizo Mratibu wa Huduma za Afya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kiteto, Saraweki Mbelwa, amesema huo ni mwendelezo wa jitihada za kuwaepusha watu na upofu kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa Mvumi Dodoma.

Amesema matatizo yanayoyawasumbua watu wengi wa umri mkubwa ni mtoto wa jicho, mtindio wa maji kwenye macho, vikope na vidonda kutokana na kuumia kwenye macho.

"Upofu unachukua asilimia 1.3 ya wananchi wote, tumeshawafikia watu laki saba kwa kuwafanyia operesheni kubwa na ndogo wapatao laki tano," amesema Mbelwa.

Baadhi ya wananchi wa Kiteto waliofanyiwa upasuaji kuondoa mtoto wa jicho.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, tangu mwaka 2016 hadi 2023 wakazi 700,000 wa Kiteto na wilaya za jirani wamefanyiwa upasuaji wa macho kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Mvumi Dodoma.

"Kituo cha Afya cha Anglikana Dayosisi ya Kiteto tunashirikiana na madaktari bingwa kutoka Mvumi Dodoma kufanya operesheni za matatizo ya macho, tatizo hili bado ni kubwa kwa ukanda wa Kiteto na Simanjiro," amesema Mbelwa.

Mmoja wa wanufaika wa huduma hiyo na mkazi wa Kijiji cha Ngipa, Isaya Malogo, amesema tatizo la macho lilimfanya hata ulaji wake kuwa mgumu.

"Nilikuwa sioni kabisa nikapata taarifa kutoka kwa majirani zangu kwamba kuna huduma inayotolewa Kibaya Kiteto ndipo nikapata dawa na kufanyiwa operesheni, nashukuru sana sasa naweza kutambua hata watu," amesema Malogo.

Mkazi wa Kijiji cha Sagala Kongwa, Veronica Samamani, amesema
awali alikuwa akilima lakini baada ya kupata tatizo alilazimika kubaki nyumbani ambapo amekuwa akifanyiwa kila kitu na watu.

Mchungaji George Nghongolo wa Kijiji cha Matui, amekipongeza kituo hicho na Hospitali ya Mvumi kwa huduma hizo ambazo zitawawezesha ndugu zao kufanya shughuli za maendeleo.

"Mimi ni mchungaji kuna wakati nilikuwa naacha majukumu yangu mbalimbali kwa ajili ya kumuhudumia baba yangu, nafurahi sana Mungu amemponya," amesema Mchungaji Nghongolo.
Powered by Blogger.