SHEIKH JALALA: UMOJA WA WATANZANIA NI MUHIMU

 Mwenyekiti wa wanawake

Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna’shariyyah, Hemed Jalala, akizungumza na vyombo vya habari wakati wa matembezi ya amani kuenzi matendo mema yaliyofanywa na Mjukuu wa Mtume, Imam Hussein.


Na Nora Damian

Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna’shariyyah, Hemed Jalala amewataka Watanzania kuenzi na kudumisha amani iliyopo kuepuka nchi kuingia kwenye machafuko.

Ameyasema hayo Dar es Salaam Julai 28,2023 wakati wa matembezi ya amani kuenzi matendo mema yaliyofanywa na Mjukuu wa Mtume, Imam Hussein, ambaye aliuawa akipigania haki.

“Dunia hii kuna watu wanafanya mbinu za kuondoa amani tuliyonayo, moja ya malengo yetu makubwa ni kuboresha amani yetu. Nchi jirani wenzetu hawatulii kwa sababu wamekosa amani…tuendelee kuenzi amani ya Tanzania na kuhakikisha inabakia kuwa kisiwa cha amani,” amesema Sheikh Jalala.

Waumini wa Jumuiya ya Shia Ithna’shariyyah Tanzania wakiwa kwenye matembezi ya amani  kuenzi matendo mema yaliyofanywa na Imam Hussein.

Akizungumzia matembezi hayo amesema ni ishara kwamba wako tayari kumuunga mkono Imam Hussein kwa vitendo.

“Mafunzo yake ya uhalisia alikuwa anahimiza utu na tutayahimiza katika mwaka huu wa 1445, tunahimiza somo la watu kupendana, kushirikiana na kushikamana.

“Turudishe upendo kwa Watanzania wote, Masuni na Mashia wapendane, waelewane, wakae vizuri na wenzao, wawe ni Wayaudi, Wakristo ama Wapagani,” amesema.

Kwa mujibu wa Sheikh Jalala, Imam Hussein alihimiza kuthamini utu, ubinadamu, huruma, upendo, heshima na kujitolea kuwatumikia watu na kutetea amani.

Mwenyekiti wa Wanawake Jumuiya ya Shia Ithna'ashariyyah Tanzania, Fatma Mwiru, akizungumza na vyombo vya habari wakati wa matembezi ya amani kuenzi matendo mema ya Imam Hussein.

Mwenyekiti wa Wanawake Jumuiya ya Shia Ithna’shariyyah Tanzania (TIC Taifa), Fatma Mwiru, ameitaka jamii ijifunze kujitoa kwa ajili ya wengine na kuacha ubinafsi.

“Imam Hussein alijitoa kwa watu wote kutetea haki zao, kubwa tunalojifunza ni kujitoa kwa ajili ya wanyonge, tuache ubinafsi hasa viongozi ukijitoa jina lako litabaki salama.

“Tunamshukuru Rais Samia amewapa kipaumbele wanawake katika uongozi wake kwa sababu anatambua mwanamke ana mchango mkubwa kwenye jamii,” amesema Fatma.

Matembezi hayo pia yalikwenda sambamba na uchangiaji damu ambapo waumini na viongozi mbalimbali wa jumuiya hiyo walijitolea kusaidia watu wenye uhitaji.










 T.I.C Taifa

Powered by Blogger.