TANESCO YATENGENEZA FAIDA YA SH BILIONI 109



Mkurugenzi wa Shirika la Umeme, Maharage Chande, akizungumza wakati wa kikao kazi cha uongozi wa Tanesco, Msajili wa Hazina na Wahariri wa Vyombo vya Habari, Dar es Salaam.

Na Nora Damian

Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) limepata faida ya Sh bilioni 109 kwa mwaka 2021/22 ambazo zimeongezeka kutoka Sh bilioni 77 mwaka 2020/21.

Shirika hilo lenye wateja milioni 4 kwa mwaka 2021/22 limefanikiwa kuwaunganishia umeme wateja wapya 504,366 huku upotevu wa umeme ukipungua kutoka asilimia 9 mpaka 8.

Mafanikio hayo yameelezwa leo Julai 27,2023 na Mkurugenzi wa Fedha, Renata Ndege, wakati wa kikao kazi cha uongozi wa Tanesco, Msajili wa Hazina na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

“Sasa hivi shirika letu sio lile linalotengeneza hasara tena ni shirika linalotengeneza faida, mambo mengi yamevunja rekodi ambayo haijapata kutokea, mwaka jana tuliweka vigezo vya kupimana kufanya kazi, kwa mfano kuunganisha wateja, tunatatua matatizo yao na tunatoa taarifa.

“Sasa hivi tunapimana na ndio maana huduma imeboreka…hatujafika tunakotaka lakini huduma imeboreka sana,” amesema Ndege.


Mkurugenzi wa Fedha Tanesco, Renata Ndege, akizungumza wakati wa kikao kazi cha uongozi wa shirika hilo, Msajili wa Hazina na Wahariri wa Vyombo vya Habari, Dar es Salaam.

Amesema pia mauzo ya umeme yameongezeka kutoka Sh trilioni 1.6 mwaka 2020/21 na kufikia Sh trilioni 1.8 mwaka 2021/22 ambayo yalikua kwa asilimia 11.

Kuhusu kutoa gawio serikalini Mkurugenzi wa shirika hilo, Maharage Chande, amesema bado lina mawanda makubwa ya kupeleka umeme hivyo fedha zinazopatikana zinaelekezwa katika miradi ikiwemo kupeleka umeme mikoa mbalimbali.

“Mara nyingi unakuta kwamba tunapata faida lakini zile fedha tunatumia kuziwekeza katika miundombinu,” amesema Chande.

Mkurugenzi huyo amesema kukamilika kwa miradi mbalimbali inayoendelea kutaongeza uzalishaji na kupunguza gharama ukiwemo wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambao umefikia asilimia 90 huku wakitarajia kuwasha umeme Juni 2024.

Kwa mujibu wa Chande, kila mwaka huchagua wafanyakazi 20 wenye weledi kisha kuwapeleka nje ya nchi na kuwaunganisha kwenye kampuni kubwa ambapo 20 wanaendelea na mafunzo Afrika Kusini.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amelipongeza shirika hilo kwa maboresho makubwa na kushauri itafutwe tiba ya kudumu kwa matatizo mengine yanayolikabili.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile.
 
“Kasi ya mabadiliko ndani ya Tanesco inaonesha taasisi hii imejipanga na inaweza kuwa ya mfano…Tanesco kutoka shirika la kupata hasara linastahili pongezi,” amesema Balile.

Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia kikao kazi kilichohitishwa na uongozi wa Tanesco na Msajili wa Hazina, Dar es Salaam.





Powered by Blogger.