WIKI YA AZAKI 2025 KUADHIMISHWA ARUSHA, STANBIC WATIA MGUU

Na Nora Damian, The Page

Maadhimisho ya saba ya Wiki ya Azaki yanatarajiwa kufanyika jijini Arusha na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili njia zitakazoweza kutumika katika kuyaelekea maendeleo.

Wiki hiyo inayoratibiwa na Asasi ya Foundation for Civil Society (FCS) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mashirika inalenga kujadili masuala ya kijamii na maendeleo. 

Akizungumza Mei 22,2025 na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge, amesema wiki hiyo itawakutanisha wadau wa maendeleo kutoka kila kona kujadili njia zitakazoweza kutumika katika kuyaelekea maendeleo.

"Wiki ya Azaki itahusisha mijadala kuhusu masuala mengine ya kimaendeleo kama kujadili njia mbadala za kukuza wajasiriamali, majadiliano kuhusu demokrasia nchini pamoja kujadili kuhusu suala zima la ubia wa maendeleo.

“Wiki ya Azaki itajikita kujadili njia za kupita katika kuielekea dira ya taifa ya maendeleo. Tukio hilo litahusisha wadau wa maendeleo kutoka taasisi mbalimbali watakaokutana kushiriki mijadala mbalimbali,” amesema Rutenge.

Nesia Mahenge ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Azaki nchini na Mkurugenzi Mkazi wa taasisi ya kimataifa iliyojikita kuimarisha mifumo ya maisha kwa jamii ya watu wenye ulemavu (CBM, Christian Blind Mission), amesema kupitia maadhimisho hayo wadau kutoka sekta mbalimbali watapata fursa ya kujifunza namna watakavyoweza kuchangia katika kuleta maendeleo nchini.

“Tunashirikiana na Serikali kwa karibu ili iweze kutuongoza vyema katika kujadili maendeleo nchini,” amesema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Taasisi za Umma na Mashirika Binafsi kutoka Benki ya Stanbic, Doreen Dominic, amesema ushiriki wao katika tukio ni sehemu ya dhamira yao ya kuchochea maendeleo ya jamii.

Amesema benki hiyo itachangia Sh milioni 40 kama sehemu ya kuchochea maendeleo ya jamii kwa ushirikiano wa kweli.Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Tanzania Bora, Ismail Biro, ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kuthibitisha ushiriki wao katika wiki hiyo ya Azaki.

Maadhimisho ya Wiki ya Azaki yanatarajiwa kufanyika Juni 2 mpaka Juni 6 mwaka huu jijini Arusha.

Powered by Blogger.