TMA: WANANCHI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA BARIDI, VUMBI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, upepo na mvua kwa kipindi cha Juni hadi Agosti 2025 mwaka huu huku ikitahadharisha magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi.
Akizungumza leo Mei 22,2015 na vyombo vya habari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chan’ga, ametoa tahadhari na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.
"Vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria hususan Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Mara pamoja na ukanda wa pwani na maeneo ya nchi kavu (mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).
"Katika msimu wa Juni hadi Agosti 2025, joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuwa la wastani. Kwa Bahari ya Hindi, joto la Bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya mashariki (pwani ya Indonesia), wakati joto la bahari la wastani linatarajiwa katika maeneo ya magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika Mashariki). Hali hizi za bahari kwa pamoja zinatarajiwa kuwa na mchango hafifu katika mifumo ya hali ya hewa hapa nchini," amesema Dkt. Chang'a.
Aidha amesema joto la bahari katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi (kusini mwa Madagascar) linatarajiwa kuwa la juu ya wastani na kwamba hali hiyo inatarajiwa kudhoofisha mgandamizo mkubwa wa hewa katika eneo hilo na hivyo kupunguza kasi ya upepo wenye baridi kutoka kusini kuelekea katika maeneo ya nchi yetu.
Vilevile amesema vipindi vichache vya upepo unaovuma kutoka msitu wa Congo kuelekea maeneo ya magharibi mwa nchi vinatarajiwa. Hali hii inatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua kwa baadhi ya nyakati hususan katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.
"Katika msimu huu, magonjwa yanayohusiana na hali ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza hususan maeneo ya magharibi mwa nchi, nyanda za juu kusini magharibi na baadhi ya maeneo ya kati mwa nchi ingawa kwa kiasi kidogo.
"Pia vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho na magonjwa mengine yanayohusiana na hali hiyo. Upungufu wa maji na malisho unaweza kujitokeza katika baadhi ya maeneo," amesema.
Ameshauri tahadhari za kiafya zichukuliwe ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi.
"Kutokana na hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi katika kipindi hiki, maji na malisho yanapaswa kutumika kwa uangalifu ili kupunguza athari zinazotarajiwa.
"Wafugaji wanashauriwa kuendelea kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo ili kudhibiti magonjwa ya mifugo na kufuata ushauri wa wataalam. Wakulima wanashauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo oevu na pia katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hiki cha msimu wa Kipupwe," amesema.
Dkt. Chang'a ameshauri watumiaji wa bahari kufuatilia taarifa za hali ya hewa zikiwemo utabiri wa kila siku, angalizo na tahadhali ili kuongeza ufanisi na usalama wa shughuli za baharini, na kupunguza athari za upepo mkali unaotarajiwa.
Hata hivyo, amesema sekta za ujenzi, madini na uchukuzi zinatarajiwa kunufaika kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa.
Mamlaka hiyo imesema itaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejesho.
