WAFANYAKAZI BORA HOSPITALI YA TEMEKE WAELEZA SIRI YA MAFANIKIO
Na Nora Damia, The Page
Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) zimeleta kicheko katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke baada ya watumishi watatu wa hospitali hiyo kuchukua tuzo ya wafanyakazi bora.
Watumishi hao ambao wametangazwa wakati wa sherehe zilizofanyika kimkoa katika viwanja vya Tanganyika Packers, jijini Dar es Salaam ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Emmanuel Lazaro, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Abdallah Mashombo na Muuguzi Mkunga, Dorothy Hokororo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa cheti na fedha taslimu Sh milioni 5, Dkt. Lazaro amesema siri ya mafanikio ni kufanya kazi kwa bidii na kuwapenda unaowahudumia.
"Naishukuru Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke kwa kuniona katika utendaji wangu, kikubwa ni kufanya kazi kwa bidii na kuwapenda wale unaowahudumia. Nitaendelea kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya taifa letu," amesema Dkt. Lazaro.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Dkt. Joseph Kimaro, amesema tuzo zinazotolewa wakati wa Mei Mosi zinaleta chachu ya kuhamasisha watumishi wengine kufanya kazi vizuri na kwa weledi katika kuhakikisha kwamba wanatoa huduma bora.
"Katika mwaka huu wa fedha tumeshuhudia mabadiliko na maboresho mengi katika hospitali yetu na hii yote tunapeleka sifa kwa Serikali chini ya mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi wake mzuri pamoja na Wizara ya Afya.
"Tumeweza kuanzisha huduma mpya ya 'Endoscopy' ambayo mara nyingi watu wa Temeke walikuwa wanaitegemea Muhimbili, tumeboresha huduma za watoto wachanga kuanzia anapozaliwa hadi siku 28, pia tumeweza kuboresha sana utoaji huduma kwa kina mama.
"Ukiangalia mwaka 2021/2022 kipindi kama hiki tulikuwa tumeshapoteza kinamama kumi lakini kwa mwaka huu kwa bahati mbaya sana tumepoteza akinamama wawili tu...kwahiyo uwekezaji wa Serikali unafanya kazi nzuri na unatafsirika kwenda kwenye huduma bora na kupunguza vifo vya kinamama na watoto wachanga," amesema Dkt. Kimaro.
Amesema watumishi wa hospitali hiyo wameona matunda ya kufanya kazi kwa kujituma na kwa weledi na kuwasihi kuiga mfano ulioonyeshwa na wenzao kwa kufanya kazi kwa kujituma huku wakifuata taratibu zote za kisheria na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa kuzingatia miongozo yote.
"Waweze kuzingatia kwamba kila wakati wanapotoa huduma kwa mgonjwa yeyote watoe huduma kama vile ambavyo wao wangeweza kuhudumiwa," amesema Dkt. Kimaro.
