WANANCHI LUDEWA WATAKIWA KUWA MABALOZI UHIFADHI WA MISITU

Na Happiness Shayo, Ludewa

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana amewataka wananchi Ludewa kuwa mabalozi katika uhifadhi wa misitu na mazingira na kudhibiti moto kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye. 

Ameyasema hayo leo Aprili 18,2025 alipokuwa akifungua semina ya kujengeana uwezo kuhusu uhifadhi wa misitu na mazingira na njia za kuzuia na kudhibiti moto iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Ludewa, mkoani Njombe.

“Misitu yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uchomaji moto holela na ukataji wa miti hovyo kwa matumizi mbalimbali ya kibinadamu kama vile uandaaji wa mashamba, kuchoma mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia hivyo, ninyi mnaopata mafunzo haya mkawe mabalozi wa kupeleka elimu mtakayoipokea hapa kwa wananchi mnaowaongoza ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika shughuli za uhifadhi na utunzaji wa mazingira," amesisitiza Dk. Chana. Amefafanua kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za utatuzi ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara, kutoa elimu ya kuzuia uchomaji wa moto na kugawa miche ya miti na mizinga ya nyuki katika maeneo mbalimbali yanayozungukwa na misitu.

Waziri huyo ametoa rai kwa halmashauri za wilaya kuwa na utaratibu wa kujadili mara kwa mara masuala ya uhifadhi wa misitu, utunzaji wa vyanzo vya maji na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla kwani kwa kufanya hivyo ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hasan katika kuhifadhi mazingira kwa kutokata miti na kutumia nishati safi ya kupikia.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, amesema mafunzo hayo yataongeza tija katika utunzaji wa mazingira na misitu hasa kiuchumi na kwamba halmashauri itatoa ushirikiano kuhakikisha malengo ya uhifadhi yanafikiwa.Semina hiyo imehudhuriwa na viongozi wa chama na Serikali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, madiwani, wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau mbalimbali wa uhifadhi kutoka kata za Wilaya ya Ludewa.

Powered by Blogger.