TAHADHARI MUHIMU ZA AFYA ZA KUZINGATIWA SIKUKUU YA PASAKA

Afisa Afya na Mazingira Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke, Juhudi Nyambuka ametoa tahadhari kwa wananchi hasa wanaofika katika hospitali hiyo kuendelea kuchukua tahadhari za afya hasa katika kipindi hiki cha sikukuu za Pasaka.

Amesema eneo muhimu zaidi la kuzingatia ni katika ulaji wa vyakula ambapo amewasihi kuhakikisha chakula kinaandaliwa na kuliwa katika mazingira ya usafi ili kuzuia hatari ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na maambukizi mengine yanayosababishwa na ulaji wa vyakula ambavyo si safi na salama.

Amesema magonjwa mengi ya mlipuko ikiwemo kipindupindu chanzo chake huanzia na vyakula ambavyo watu wanakula ambapo kwa kiasi kikubwa katika kipindi kama hiki cha sikukuu watu huwa na utaratibu wa kila vyakula mbalimbali pasipokuangalia usalama wa vyakula hivyo.

Pia amesisitiza umuhimu wa kunawa mikono kabda ya kula chakula, unapotoka msalaani lakini pia kuosha vizuri matunda yoyote kabda ya kuyatumia iwe ni matunda kwa ajili ya juisi au yenyewe.

Amesema watoto wanapaswa pia kupewa uangalizi zaidi kuhakikisha chochote wanachokula kinakuwa katika hali ya usafi ambapo kwa kufanya hivyo watahakikisha wanakuwa salama dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Amewasisitiza pia kuendelea kuchukua tahadhari za kiusalama dhidi ya vyombo vya moto kwa sababu msimu wa sikukuu kunakuwa na matukio mengi yanayosababisha kutokea kwa ajali nyingi hivyo, ni muhimu kila mmoja kuhakikisha anakuwa salama katika kutumia barabara ili kupunguza ajali na idadi ya majeruhi wanaopokelewa hospitali msimu huu wa sikukuu.Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke itaendelea na utaratibu wake wa kila siku wa kutoa huduma kwa wananchi hata katika msimu huu wa sikukuu huduma zote zinaendelea kutolewa.

Powered by Blogger.