TMA YAPONGEZWA KWA UBORESHWAJI TAARIFA ZA HALI YA HEWA
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepongezwa kwa uboreshwaji wa utabiri wa hali ya hewa na taarifa za tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini.
Hayo yamesemwa Aprili 15,2015 na Dkt. Rozalia Rwegasira, Kaimu Katibu Tawala Mkoa, sehemu ya uchumi na uzalishaji wa mkoa wa Morogoro wakati wa ufunguzi wa Semina ya Mradi wa kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na matukio ya hali mbaya ya hewa na kupunguza hasara na uharibifu.
“Utabiri wa hali ya hewa umeendelea kuboreshwa na tahadhari za mvua kubwa na matukio ya hali mbaya ya hewa zinatolewa kwa wakati hivyo, kuchangia kuokoa maisha ya watu na mali zao. Tunaishukuru na kuipongeza serikali kwa kupitia TMA kwa kazi hii njema," amesema Dkt. Rozalia.
Aidha ametoa ahadi ya kushirikiana na TMA katika kufanikisha utekelezwaji wa mradi huo kwani utakuwa na faida kubwa na chanya kwa wananchi wa Tanzania.
“Katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huu, kwa niaba ya ofisi ya mkuu wa mkoa tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wananchi wananufaika na taarifa zitakazozalishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia nradi huu, ili wadau na wananchi kwa ujumla kuweza kuchukua tahadhari kwa lengo la kupunguza athari zitokanazo na matukio ya hali mbaya ya hewa," amesema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa nchini.
“Nitumie fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza na kuisaidia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini kwa kuweka sera, mikakati na mazingira wezeshi yanachochea ubunifu na umahiri," amesema.
Dkt. Chang’a amesisitiza kwamba uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu ya hali ya hewa nchini ndio chanzo kikuu cha uboreshwaji wa taarifa za hali ya hewa nchini na kuwasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari zinazotolewa na TMA, pia kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa namba 2 ya mwaka 2019 na kanuni zake.
Mamlaka ya hali ya hewa inatoa shukrani za dhati kwa Tume ya sayansi na teknolojia (COSTECH) kwa kufadhili mradi huo muhimu ambao utaongeza ufanisi katika mchakato wa kukabiliana na mabadiliako ya hali ya hewa na tabianchi nchini.
