TANAHUT WATAKA HATUA ZAIDI KUDHIBITI USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU

*Wasema Taifa linapoteza nguvu kazi


Na Nora Damian, The Page 

Mtandao wa Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu (TANAHUT) umeishauri Serikali kuhakikisha visa vyote vya usafirishaji haramu wa binadamu vinapelelezwa kwa weledi na kupelekwa mahakamani ili wahalifu waadhibiwe na wahanga wapate haki zao. 

Wito huo umetolewa leo Aprili 15,2025 na Mkurugenzi wa TANAHUT, Wakili Edwin Mugambila, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usafirishaji haramu wa binadamu nchini. 

Amesema wamekuwa wakiibua matukio mbalimbali ya usafirishaji haramu wa binadamu lakini hatima za wahanga huwa hazijulikani.

Mtandao huo umedai kuwapo kwa baadhi ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo wakiwemo viongozi wa dini, kampuni zinazohusika kuwatafutia vijana ajira, watumishi wa Serikali wasiokuwa waaminifu hasa wa idara ya ustawi wa jamii.“Kuna makampuni yamechukua vijana zaidi ya 1,000 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wengine wakiwa ni wanafunzi wa vyuo na waliomaliza kidato cha nne, wanawadanganya kuwa wanatoa ajira, nafasi za kusoma na fursa za biashara mtandaoni. 

“Huwapangishia vyumba maeneo mbalimbali na kuwatumikisha kutekeleza uhalifu wa kitapeli, vijana hushurutishwa kuwadanganya wazazi kwamba wamepata ajira na nafasi za kwenda kusoma nje ya nchi na kuwataka wazazi kulipa gharama za safari kama njia ya kujipatia fedha za kujiunga na kampuni. 

“Hutumikishwa kwa shurti, hawapewi uhuru bianfsi na kila fedha inayopatikana inakwenda kwa viongozi wao na hawalipwi, badala yake hupewa vitisho iwapo watatoroka ama kusema popote,” amesema Wakili Mugambila. 

Mtandao huo umeitaka Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu (ATC) kusimamia vizuri majukumu yake kwa kuzingatia kifungu cha 30 cha Sheria ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu.




Powered by Blogger.