MBIO ZA RUN FOR BINTI 2025 KUJENGA VYOO BORA GEITA, DAR

Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng'wanakilala, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimu wa nne wa mbio za Run for Binti.


Na Nora Damian, The Page

Msimu wa nne wa mbio za Run for Binti unatarajia kuwafikia wanafunzi 2,800 katika shule tatu za Mikoa ya Dar es Salaam na Geita ambao watajengewa vyoo bora, kupatiwa taulo za kike na hifadhi ya mazingira.

Mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Mei 24,2025 katika viwanja vya Farasi, Oysterbay jijini Dar es Salaam zimeandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika lisilo la kiserikali lililojikita katika kukuza upatikanaji wa haki kwa wote (LSF) na Shirika la Smile for Community (S4C).

Akizungumza leo Aprili 16,2025 wakati wa kutangaza mbio hizo, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng'wanakilala, amesema kupitia mbio hizo wanapunguza vikwazo na kutengeneza njia mpya zitakazochochea jamii yenye usawa hususan kwa mtoto wa kike."Mbio hizi hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuweka nguvu na rasilimali za pamoja katika kuwawezesha watoto wa kike kupata haki ya elimu na afya ya uzazi, kwa kuhakikisha wanapata hedhi salama na mazingira bora ya kusoma.

"Kupitia Run for Binti ya mwaka jana wanafunzi wa Shule za Sekondari Nanyamba na Chawi katika Halmashauri ya Mji Nanyamba walinufaika kwa kujengewa vyoo bora na vya kisasa, huku wanafunzi wa kike wakipata taulo za kike kwa ajili ya kuwalinda kiafya na kuwawezesha kuhuchuria vipindi bila kukosa," amesema Ng'wanakilala.

Aidha amesema katika utekelezaji wa mradi wa Sauti ya Mwanamke nchini, wameona wasichana na mabinti wanakumbana na vizuizi vinavyozuilika na visivyoweza kuzuilika katika kupata elimu, huduma za afya na haki zao za msingi ndiyo maana ushirikiano wao na Smile for Communty pamoja na wadau mbalimbali ni muhimu kutatua changamoto hizo. 

Mwaka jana zaidi ya wanafunzi 2,500 walinufaika kupitia ujenzi na ukarabati wa vyoo, usambazaji wa taulo za kike, upandaji wa miti mashuleni na utoaji wa elimu ya hedhi salama na haki za moto wa kike.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Smile for Community, Flora Njelekela, amesema lengo la mwaka huu ni kufikia watoto wa kike 1,000 kutoka shule tatu, hasa mikoa ya Geita na Dar es Salaam.Amesema pia watasambaza taulo za kike 7,000, ujenzi wa vyoo bora mashuleni, upandaji wa miti 500 katika shule tatu kwa ajili ya hifadhi ya mazingira.

Pia itatolewa elimu ya ukatili wa kijinsia na mbinu za kuzuia na kushughulikia matukio hayo, elimu ya fedha (financial literacy) na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na shughuli za mazingira zitafanyika Ukonga Dar es Salaam na shughuli za afya ya hedhi, elimu ya fedha na miundombinu Geita.

Mbio hizo zitahusisha wakimbiaji watahusika katika mbio za komita 21, kilomita 10 na kilomita 5.


Powered by Blogger.