KUPATA MTOTO KATIKA UMRI MKUBWA KUNAWEZA KUSABABISHA KUZALIWA MWENYE USONJI

 

Na Nora Damian, The Page

Wakati Tanzania ikikadiriwa kuwa na watoto 20,000 wanaozaliwa na tatizo la usonji kila mwaka, inaelezwa kuwa kupata mtoto katika umri mkubwa ni mojawapo ya visababishi vya ugonjwa huo. 

Kulingana na wataalam wa afya, usonji ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa fahamu na ukuaji na kusababisha hali ya upekee inayohusiana na utofauti katika namna mtu anavyofikiri, anavyojifunza na jinsi anavyohusiana na wengine. 

Hali hiyo pia inaweza kuambatana na magonjwa mengine ya akili na mfumo wa fahamu ikiwemo kifafa au 'hali ya kukosa utulivu' (ADHD) na kwa baadhi ya wagonjwa kuwa na uwezo wa chini kabisa wa ufahamu. 

Apliri 2 kila mwaka ni Siku ya Usonji Duniani na leo Tanzania imeungana na mataifa mengine kuadhimisha huku msisitizo mkubwa ukilenga kuhamasisha jamii kuhusu uelewa juu ya uwepo wa tatizo hilo.

Dk. Omary Ubuguyu ni Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa Yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya, ambaye amesema kisababishi hasa cha tatizo hilo inadhaniwa kuwa ni matokeo ya mchanganyiko wa vinasaba na visababishi vya kimazingira.

"Kupata mtoto katika umri mkubwa ni miongoni mwa vitu ambavyo vinaonesha kwamba vinaweza kuchochea kupatikana kwa ugonjwa wa usonji. Na umri mkubwa si wa mama tu, wa baba pia unaonekana unachochea zaidi kuliko hata wa mama.

"Hata vinasaba vilivyobadilika kutoka kwa baba aliyeishi umri mkubwa zaidi inaweza ikachochea," amesema Dk. Ubuguyu.

Amesema pia wapo watu wenye usonji ambao tatizo kubwa linabaki kwenye mawasiliano na mahusiano pekee, bila ya kuonesha dalili yeyote ya ugonjwa. 

"Dalili za kwanza za usonji huonekana kabla ya mtoto kufikia umri wa miaka mitatu na kabla ya umri huo," amesema.

Kwa mujibu wa Dk. Ubuguyu, mpaka sasa Serikali imesajili watoto 1,416 ambao wanapata huduma katika shule 18 maalumu zenye walimu 157.Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amesema Serikali imeanzisha mafunzo ngazi ya Diploma ili kuongeza wahitimu wenye ujuzi na weledi ambao watatoa elimu kwa watoto wenye changamoto za usonji nchini. 

Amesema mafunzo hayo yanayojumuisha mbinu na mikakati ya kufundisha watoto wenye usonji, kutambua dalili za usonji, na jinsi ya kuwasiliana na watoto wenye usonji yanatolewa katika Chuo cha Ualimu Patandi Arusha.

"Ingawa hatuwezi kuzuia wazazi kupata mtoto mwenye usonji, tunaweza kuongeza uwezekano wa kupata watoto wenye afya nzuri kwa kufanya mabadiliko muhimu katika mtindo wa maisha.

"Hii ni pamoja na kula mlo bora, kufanya mazoezi mara kwa mara na kuhakikisha uchunguzi wa afya kabla na wakati wa ujauzito. 

"Ni muhimu kushirikiana na wataalam kuhusu matumizi ya dawa na kuepuka vinywaji vyenye kileo kama pombe, kwani vinaweza kuathiri ukuaji wa mtoto na kuongeza hatari ya matatizo ya kiafya, ikiwa ni pamoja na ulemavu wa mfumo wa fahamu," amesema Dk. Mollel.

Dk. Mollel ametoa wito kwa jamii kutowaficha watoto wenye changamoto hizo na kuwataka wazazi na walezi kuwasiliana na wataalamu ili kupata elimu na kujifunza jinsi ya kuwatunza watu wenye usonji na kuwawezesha kujisimamia katika maisha yao ya kila siku.














Powered by Blogger.