KAMATI TENDAJI MRADI WA SOFF KUTATHMINI UTEKELEZAJI MPANGO KAZI ULIOIDHINISHWA
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Imeelezwa kuwa moja ya masuala yatakayojadiliwa katika kikao cha pili cha Kamati Tendaji ya Utekelezaji Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF) ni pamoja na kutathmini utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2024, kupokea na kupitsha mpango kazi na bajeti kwa mwaka 2025.
Hayo yamesemwa Aprili 10,2025 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, wakati akifungua mkutano wa pili wa kamati hiyo mkoani Morogoro.
Dkt. Chang’a ameishukuru kamati hiyo pamoja na sekretarieti kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kuhakikisha majukumu ya mradi kwa mwaka 2024 yanatekelezwa kwa ufanisi ikiwemo hafla ya uzinduzi wa mradi huo.
Amefafanua kuwa TMA iliandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maelekezo matano yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa uzinduzi yakiwemo masuala ya utekelezaji wa shughuli za mradi kwa wakati na ufanisi pamoja na ushirikiano baina wa wadau wa mradi.
Awali Naibu Mwakilishi Mkazi Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Amos Manyama, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania, TMA na wadau wengine wa mradi kuhakikisha malengo ya SOFF yanafikiwa.
Aidha amesisitiza haja ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na TMA katika kuimarisha huduma za hali ya hewa hata baada ya mradi
Katika hatua nyingine, Kamati ilipokea na kuidhinisha Mpango Kazi wa mwaka 2025, taarifa ya hesabu kwa mwaka 2024 na Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi.
SOFF ni Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa kwa Nchi zinazoendelea na Nchi za Visiwa vidogo.
Lengo la mradi ni kuimarisha huduma za hali ya hewa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ili kulinda maisha ya watu na mali ikiwemo kuboresha zaidi miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na kuhakikisha Tanzania inakidhi mahitaji ya wadau wa kitaifa na kimataifa.
Mradi huo unatekelezwa kwa muda wa miaka minne kuanzia Julai 2024 hadi Desemba 2027.
