JERRY SILAA: TUSIICHEZEE AMANI TULIYONAYO

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Tamasha la Mtoko wa Pasaka, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amewataka Watanzania kulinda na kuienzi amani iliyopo kuepuka nchi kuingia kwenye machafuko.

Waziri Silaa ameyasema hayo leo Aprili 20,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Tamasha la Mtoko wa Pasaka linalofanyika jijini Dar es Salaam.

"Amani iliyopo ni tunu kubwa ambayo inatakiwa kutunzwa, ukiangalia mitandaoni utaona adha ambayo wanaipata wananchi ambao nchi zao zina machafuko, utaona kuwa amani tuliyonayo si ya kuichezea," amesema Silaa.

Aidha amesema tamasha hilo lenye kaulimbiu 'Kwa maombi utashinda' ni kielelezo cha jitihada za kuendelea kuitunza amani iliyopo nchini.

Tamasha hilo lililoandaliwa na Mwanamuziki wa Injili, Christina Shusho, linahusisha pia kuliombea Taifa na linashirikisha wanamuziki mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. 

Miongoni mwa wadhamini katika tamasha hilo ni taasisi ya Mama Ongea na Mwanao inayoongozwa na Steve Nyerere.


Powered by Blogger.