DKT. NCHIMBI AHUBIRI NGUVU YA MSAMAHA, MAOMBI SIKUKUU YA PASAKA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, akizungumza wakati wa tamasha la Mtoko wa Pasaka lililofanyika ukumbi wa The Super Dome Masaki, Dar es Salaam.
Na Nora Damian, The Page
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi amewataka wasanii wa injili kuwakumbusha wanasiasa kuomba msamaha wanapoona wameteleza kwa kutoa maneno ambayo yataleta taswira mbaya katika taifa.
Dkt. Nchimbi amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakijisahau na kutoa maneno ambayo wakati mwingine yanakuwa mbegu ya uharibifu katika taifa hali ambayo imesababisha mataifa mengine kuingia kwenye vita.
Dkt. Nchimbi ameyasema hayo Jumapili usiku Aprili 20,2025 kwenye tamasha la Mtoko wa Pasaka lililofanyika ukumbi wa The Super Dome Masaki, Dar es Salaam.
“Mwaka huu ni mwaka uchaguzi, vyama vingi vitashiriki katika uchaguzi, nawasihi sana msiache kutukumbusha sisi wanasiasa, tukishakuwa kwenye vipaza sauti wakati mwingine tunajisahau wakati mwingine yale tunayoyasema yanakuwa mbegu ya uharibifu katika taifa, wakati mwingine unasema jambo ambalo huwezi kurudi kusema sikusema, na imetokea nchi na nchi zimeingia kwenye vita, familia zimeingia kwenye vita, koo zimeingia kwenye vita kwa jambo ambalo msemaji hakukusudia, aliteleza tu kwenye ulimi.
“Lazima tufike mahali ambapo tunaweza kuwaambia wanasiasa wetu wa CCM na vyama vingine kwamba ikitokea umeteleza bahati mbaya umesema maneno ambayo unafikiri yataleta mbegu mbaya katika taifa usione aibu kusema samahani nilikosea.
“Kwa Watanzania niwaombe sana mtu yeyote akitoka akasema mbele ya umma kwamba anaomba radhi alikosea tusimuone ni mdhaifu, hii ndiyo aina ya watu ambao tunawataka katika taifa hili…watu ambao hawaoni taabu kudhalilika, kujishusha ili taifa lipone,” amesema Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi pia amewahimiza waumini wa dini zote kuendelea kuliombea taifa na viongozi wake ili liendelee kuwa imara na lenye mshikamano.
Amesema viongozi wote wa Tanzania wakiwemo wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi za umma, mashirika mbalimbali, familia waingizwe kwenye maombi endelevu ili nchi ijivunie historia itakayokuwa nayo katika wakati huo.
“Kwa maombi tutashinda, Tanzania tutashinda, kauliumbiu yenu inalikumbusha taifa kwamba ni kwa njia ya Mungu tu ndiyo taifa hili litaendelea kubaki, tuendelee kukumbusha waumini wa dini zote kwamba taifa hili haliwezi kuendelea kuwa taifa imara, lenye mshikamano kama Mungu hajasimama na taifa hili.
“Tusione aibu kumtanguliza Mungu katika kulisimamia, kulilinda na kulibadili taifa letu, salama ya kizazi cha sasa na kijacho inategemea sana mapenzi na uwezo wetu kutambua kwamba Mungu ndiye usalama wetu na amani yetu,” amesema.
Aidha amesema CCM kitaendelea kusimamia uhuru wa kuabudu kwa Watanzania na watahakikisha unaimarishwa.
Mwandaaji wa tamasha hilo, Christina Shusho, amesema tamasha hilo ambalo limefanyika kwa mara ya tatu mwaka huu linalenga kuwakutanisha wasanii wa injili na wadau mbalimbali wa muziki huo kutumia sanaa ya nyimbo kufikisha ujumbe kwa taifa juu ya masuala mbalimbali.
Amesema tamasha la mwaka huu limelenga pia kuliombea Taifa hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaoatarajiwa kufanyika Oktaba mwaka huu ili ufanyike kwa amani na utulivu.
Katika hafla hiyo pia Shusho alimtangaza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, kuwa mlezi wa tamasha la Mtoko wa Pasaka kwa kuwa amekuwa akiwaunga mkono kila walipomwendea kwa ajili ya tamasha hilo.
“Wazo hili ni la Mungu na si la mtu, nilitafuta watu wanisaidie kubeba maono baba huyu (Kadogosa), hajawahi kuchoka kila nilipogonga mlango kuomba sapoti yake…tunataka kwenda na kasi ya uwezo wa SGR,” amesema Shusho.
Naye Kadogosa amemshukuru Shusho kwa heshima aliyompa na kuahidi kuwa matamasha yajayo yatakuwa mazuri zaidi ili waweze kumtukuza Mungu.


