WASIRA AWAHAKIKISHIA WANANCHI TUNDUMA KUPATIKANA UFUMBUZI KERO YA MSONGAMANO
Makamu Mwenyekiti Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewahakikishia wananchi wa Tunduma na Mkoa wa Songwe kuwa Serikali ina dhamira ya dhati kutatua changmoto zao hasa ya maji na upanuzi wa barabara.
Wasira ameeleza hayo Machi 15, 2025 alipokuwa akiwahutubia wananchi mjini Tunduma wilayani Momba Mkoa wa Songwe ambapo amesema kwa kero ya msongamano wa malori katika mji huo ufumbuzi utatokana na kupanuliwa kwa barabara ya Mbeya-Tunduma kuwa ya njia nne.
Amesema atakutana na Waziri wa Ujenzi (Abdallah Ulega) na atamfikishia ombi la wananchi wa mkoa huo kutaka upanuzi wa barabara hiyo ambao tayari umeanza mkoani Mbeya uwe na wakandarasi wawili ili mwingine aanzie Tunduma kuelekea Mbeya na hatimaye wakutane katikati kwa lengo la kuongeza kasi ya ujenzi.


