BILIONI 60 KULIPA FIDIA WANANCHI WALIOPITIWA MRADI WA RUHUDJI, RUMAKALl
NJOMBE
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kutafuta fedha za kuwalipa fidia wananchi waliopitiwa na miradi ya kufua umeme ya Ruhudji na Rumakali ili wapishe maeneo hayo na kuendelea na shughuli zao.
Kauli hiyo imetolewa Machi 16,2025 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Same, David Mathayo, baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika Mkoa wa Njombe.
“ Tayari tathmini imeshafanyika kwa wananchi watakaopitiwa na mradi huo na gharama za kuwalipa zimefahamika, wananchi wanayo taarifa, ni vyema sasa serikali ikatafuta fedha za kuwalipa fidia ili wakaendelee na maisha yao mengine wakati juhudi za kutekeleza mradi hiyo zikiendelea kufanyika,” amesema Mathayo.
Utekelezaji wa Miradi ya Ruhudji na Rumakali utaiwezesha nchi kupata zaid ya megawati 500 za umeme ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa na kuimarisha hali ya upatikanai wa umeme nchini.
Kamati hiyo imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupelekea umeme kwa wananchi wake kama alivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na kusema kuwa ni jambo la msingi kwa kuwa wananchi wamekuwa wakisubiri umeme kwa muda mrefu na kwa miaka mingi.
Alifafanua kuwa kuna maeneo mengine ni magumu kufikika kwa kuwa hakuna miundombinu ya barabara na ambayo wananchi wake walikuwa hawajawahi kupata umeme tangu enzi za uhuru, lakini kwa sasa wamepata umeme kutokana na umakini wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwajali wananchi wake.
Aidha amepongeza Wakala wa Nishati Vjijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kupelekea umeme katika vijiji na vitongoji vya mkoa huo ambapo katika maeneo mengine umefikishwa kwa asilimia 100 licha ya kuwa na miundombinu hafifu.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake wamepokea maelekezo ya kamati hiyo pamoja na shukrani kwa niaba ya serikali, katika kutekeleza miradi ya umeme.
Kuhusu suala la fidia amesema Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa wananchi wote wanaopisha miradi mbalimbali inayoanzishwa nchini, ikiwemo ya Ruhudji na Rumakali yenye thamani ya Sh bilioni 63.
Akitolea mfano baadhi ya miradi ambayo wananchi wake wamelipwa fidia ni pamoja na ule wa Tanzania - Zambia (TAZA) na mradi wa kupelekea umeme wa Gridi mkoani Katavi.
Amesema Serikali itahakikisha wananchi wanaendelea kupata umeme wa uhakika na katika Mkoa wa Njombe zaidi ya asilimia 98 ya vijiji vyote vina umeme ambapo vimebaki vijiji tisa tu ambavyo changamoto zake zinatatuliwa ili navyo vipate umeme.
Naibu Waziri huyo amesema wataendelea kusambaza umeme katika maeneo ya pembezoni na kuimarisha nguvu ya umeme ili wananchi wapate umeme mwingi wa kutosha kukidhi mahitaji yao.
Azma ya serikali ni kuhakikisha kuwa ikifikapo 2030 asilimia 75 ya wananchi wote nchini wawe wamepata umeme na waweze kutumia nishati safi ya kupikia.
“Kwa sasa Serikali iko hatua za mwisho katika kukamilisha mradi wa Julius Nyerere utakaozalisha Megawati 2,115. Azma ya Serikali ni kuhakikisha inaongeza vyanzo vya uzalishaji wa umeme hivyo inatafuta fedha ili kuanza utekelezaji wa miradi hiyo,” alisema Kapinga.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema mwambao wa Ziwa Nyasa una maeneo korofi ambayo hayafikiki kirahisi katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini kwa kuwa hakuna miundombinu ya barabara na kuahidi kutafuta mkandarasi wa kutekeleza kazi hiyo na kwamba upembuzi yakinifu unaendelea.
Amesema kazi ya kusambaza umeme katika maeneo hayo itakamilika kabla ya Juni mwaka huu ambapo vijiji vyote vitakuwa vimewashwa umeme.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Renata Ndege, amesema miradi ya Ruhuji na Rumakali itagharimu zaidi ya Sh trilioni 4.
Miradi hiyo ikitekelezwa itaongeza upatikanaji wa umeme nchini pia itaboresha maendeleo ya uchumi, ajira kwa wananchi, miundombinu ya barabara pamoja na huduma za kijamii.
