WAHIFADHI WANAWAKE TAWA WATEMBELEA PORI LA AKIBA WAMI - MBIKI

Na Joyce Ndunguru, Morogoro

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, wahifadhi wanawake wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapaori Tanzania (TAWA) wametembelea Pori la Akiba Wamimbiki lililopo katika Mikoa ya Morogoro na Pwani kwa lengo la kuhamamisha utalii wa ndani.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika Machi 1, 2025 Ofisa Mhifadhi Mkuu, Zuwena Kikoti, amesema wahifadhi wanawake wa TAWA wanaungana na wanawake wote nchini katika kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii duniani.

"Tumeungana na jitihada hizo kama wanawake kwa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Morogoro kwa lengo la kuvitangaza na kuwahamisha wanawake wa Mkoa wa Morogoro na mikoa ya jirani kutembelea hifadhi ya Wamimbiki katika kusheherekea siku ya wanawake duniani," amesema Kikoti.Naye Mwakilishi wa Kamanda wa Pori la Akiba Wamimbiki, Ofisa Utalii, Gregory Kalokole, amesema Hifadhi ya Wamimbiki ni mpya na ya kimkakati yenye vivutio vingi vya utalii ikiwemo vivutio vya asili na vivutio vya utamaduni.

"Pori la Akiba Wamimbiki lina mandhari nzuri iliyozungukwa na miti ya miombo, wanyamapori kama vile Tembo, Simba, Viboko, Chui, Fisi, Tandala, Swala pala na Kulo na asilimia takribani 20 ya Mto Wami umepita ndani ya hifadhi," amesema Kalokole.

Amewaahukuru wahifadhi wanawake kutembelea hifadhi hiyo na ametoa rai kwa makundi mbalimbali ya wanawake na Watanzania kutembela hifadhi hiyo. 

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yamepangwa kufanyika Kitaifa jijini Arusha Machi 8,2025 na kaulimbiu ya mwaka huu ni Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.


Powered by Blogger.