TAWA YASHEREHEKEA SIKU YA WANYAMAPORI KWA KUTOA MISAADA, ELIMU YA UHIFADHI

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Magharibi imesherehekea Siku ya Wanyamapori Duniani kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na uhifadhi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kulinda wanyamapori na mazingira.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Machi 3,2025 kanda hiyo ilitoa misaada ya vyakula kwa wanafunzi wenye uhitaji kutoka Shule ya Wanafunzi wenye changamoto ya uoni ya Furaha ikiwemo mchele, unga, mafuta, sukari na sabuni vyote vikiwa na thamani ya Sh millioni moja. 

Misaada hiyo imelenga kuwasaidia wanafunzi hao na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu.Vilevile TAWA ilitembelea Shule ya Sekondari Fundikila na kutoa miche 4000 ya miti ya matunda ya muda mfupi, ikihamasisha upandaji wa miti na kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira. 

Shule ya Sekondari Kanyenye nayo ilipokea miche 2000 kama sehemu ya juhudi za kukuza mazingira bora na endelevu kwa jamii.

Akikabidhi misaada hiyo na miche ya miti Kaimu Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Magharibi, Lupondije Nyanda, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora kushirikiana na Serikali katika jitihada za kulinda rasilimali wanyamapori ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira yao huku akiwahamasisha kutembelea vivutio vya utalii hususani bustani ya wanyamapori hai maarufu Tabora ZOO.

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani Kitaifa kimefanyika katika viwanja vya ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Dodoma mgeni rasmi akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana.


Powered by Blogger.