PROFESA KABUDI ASISITIZA WASANII, WAANDISHI WA HABARI KUZINGATIA MAADILI

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uzingatiaji maadili kwa wasanii na waandishi wa habari, Dar es Salaam.


Na Nora Damian, The Page

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amewataka waandishi wa habari na wasanii kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili huku akisisitiza kuwa wako tayari kulaumiwa kwa kuchukua hatua.

Ameyasema hayo leo Machi 4,2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya uzingatiaji maadili kwa wasanii na waandishi wa habari.

Amesema Serikali ina jukumu zito la kuhakikisha maadili ya Tanzania hayapotoshwi kwa namna yoyote ile na kuwataka wasanii kuiga mazuri ya tamaduni zingine na kuyaacha yale ambayo hayaendani na mila na desturi zetu."Tusiache wala kuzipuuza mila na desturi zetu nzuri maana ndizo zinazotanabaisha Utanzania wetu," amesema Profesa Kabudi.

Waziri huyo amesema vyombo vya habari ni eneo ambalo linaweza kusaidia kudhibiti mmomonyoko wa maadili kwa kuhakikisha vipindi na maudhui yanayoandaliwa yanazingatia maadili.

Aidha amesema mwaka 2022 Wizara iliandaa Mwongozo wa Maadili ya Mtanzania kama njia ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili na kwamba juhudi hizo zimeendelea kwa Baraza la Sanaa la Taifa kuchapisha mwongozo wa uzingatiwaji wa maadili katika kazi za sanaa wenye lengo la kuwaelekeza wasanii kutingatia maadili ya Kitanzania wanapotekeleza majukumu yao.

Waziri Kabudi pia amezitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Bodi ya Filamu Tanzania kuhakikisha maadili yasiyofaa hayapati nafasi na ikitokea wachukue hatua.

Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zinajadiliwa kama vile uzingatiaji wa maadili katika kazi za sanaa, maendeleo na uzalendo wa Taifa, mchango wa wasanii katika kulinda maadili ya nchi na mahusiano ya kazi za wasanii na vyombo vya habari.








Powered by Blogger.