PROFESA MKENDA: NIMEFURAHI NAANZA KUZUNGUMZA MANENO MAZURI KUHUSU VETA
Na Nora Damian, The Page
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema anaridhishwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) jinsi inavyofanyia kazi maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali.
Profesa Mkenda ameyasema hayo Machi 14,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la wadau wa Sekta ya Nguo na Mavazi lililoandaliwa na VETA kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya mamlaka hiyo.
Amesema miongoni mwa maelekezo ambayo VETA ilipewa ni kujenga mahusiano na wenye viwanda na wazalishaji na kusisitiza kuwa ni muhimu kuwe na ushirikiano katika kufanya kazi pamoja.
“Nawapongeza VETA sasa mnafanya kile tulichoagiza na nimefurahi naanza kuzungumza maneno mazuri kuhusu VETA, tunahitaji kuimarisha ushirikiano kati ya viwanda, wazalishaji na vyuo vyetu, hatuwezi kujidanganya kwamba tutapata utaalam wa mtu anatoka chuoni aje afundishe VETA bila kuwa na uzoefu wa kiutendaji,” amesema Profesa Mkenda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, amesema wataendelea kufanyia kazi maelekezo yote yanatolewa na Serikali na watahakikisha sekta hiyo inaendelea kuanzia ngazi ya ujuzi hadi sokoni.
“Kama Tanzania tuna watu karibu milioni 62 maana yake hili lote ni soko na tunatakiwa tulitumie kuzalisha bidhaa na kuziuza ndani na nje ya nchi. Ni lazima watu watambue hii ni biashara na wananchi wajivunie kuvaa mavazi yanayotengenezwa hapa nchini…tuipe kipaumbele ‘Made in Tanzania’ hususani kwenye sekta hii,” amesema Kasore.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Danford Mahwera, ambaye aliwasilisha mada kuhusu maendeleo ya sekta ya nguo na mavazi nchini, amesema nchi nyingi duniani zimeendelea kutokana na sekta ya nguo na mavazi na kwamba ni jukumu la wabunifu na vyuo kuiendeleza.
“Kuna mambo mengi katika ‘textile’ na kama mtu akisoma atajua, unaweza kujiajiri na kuna fursa nyingi. Tulipoanzisha programu hii watu walikuwa wachache, tulianza na wanafunzi saba na walipomaliza hakuna aliyebaki wote walichukuliwa,” amesema Dk. Mahwera.
Mkufunzi kutoka Chuo cha VETA Dar es Salaam ambaye aliwasilisha mada kuhusu Uwezo wa Vyuo kutoa Mafunzo Bora ya Ufundi Nguo na Ubunifu wa Mavazi, Josephat Maghina, amesema mtaala mpya uliohuishwa mwaka jana umeingiza teknolojia mpya katika ufundishaji wa masomo ya nguo na mavazi na kwamba umekidhi Sera ya Elimu ya 2014.
“Mtaala mpya umeondoa pengo lililokuwepo kati ya mtaala wa 2010 na 2015, mtaala wa sasa unawapokea wanafunzi wote. Unawakubali wanafunzi wa sekondari wanaosoma Amali na tayari tumetengeneza mlango wa ‘admission’ na hakuna atakayekataliwa,” amesema Maghina.
Mmoja wa Wataalam wa Sekta ya Nguo na Mavazi nchini, Anna Lunguya, ameipongeza VETA kwa kufanya maboresho ya mtaala ambao utawawezesha wabunifu kupata ujuzi wa kisasa na kushauri walimu waendelee kujengewa uwezo.


