TAWA YAKABIDHI MADAWATI 295 SHULE ZA MKOA WA SIMIYU

Na Mwandishi Wetu - Simiyu 

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imekabidhi madawati 295 yenye thamani ya Sh millioni 25.9 kwa shule za sekondari na msingi mkoani Simiyu.

Hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya elimu kwa shule zinazozunguka Pori la Akiba Maswa kama sehemu ya ujirani mwema kati ya TAWA na jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 7,2025 mkoani humo Ofisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja, amesema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii (Bushman Safari Trackers) wametoa madawati 295, meza mbili na viti viwili viwili kwa shule za msingi na sekondari zilizopo Wilaya za Itilima na Bariadi.Amesema Wilaya ya Itilima imepata madawati 190, meza moja na kiti kimoja na Wilaya ya Bariadi imepata madawati 105, meza moja na kiti kimoja.

Maganja amesema TAWA imekuwa na utaratibu wa kurejesha faida zinazotokana na shughuli za uhifadhi kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi zilizo chini ya usimamizi wa taasisi hiyo, na kwa Mkoa wa Simiyu madawati hayo yametokana na mapato ya shughuli za uhifadhi zinazofanyika katika Pori la Akiba Maswa.

Amewaomba wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuendelea kushirikiana na Serikali kulinda rasilimali zilizopo mkoani humo ili kuendelea kufaidi matunda yatokanayo na rasilimali hizo kwa faida ya kizazi kilichopo na vizazi vijavyo.Kwa upande wao Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Lung'wa, Exavery Mwasomola na Mwalimu Stephano Palangyo wameshukuru kwa msaada huo ambao umesaidia kutatua changamoto ya upungufu wa madawati na kuomba msaada zaidi wa kujengewa hosteli, maabara na nyumba za walimu.

Nao wanafunzi wa Shule ya Lung'wa iliyopo Wilaya ya Itilima wameipongeza Serikali kwa madawati hayo ambayo wamesema yatawasaidia kusoma kwa ufanisi zaidi na kuongeza ufaulu wao katika mitihani.

"Tumefurahi kupata msaada wa viti na madawati, kabla hatujapata madawati tulikuwa tunahangaika kukaa chini na wakati mwingine unamkuta mwanafunzi amebeba kiti chake anatembea nacho wakati wa mapumziko yote hiyo ni kutokana na uhaba wa madawati," amesema Nchama Sipewa mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Lung'wa.



Powered by Blogger.