SERIKALI YASISITIZA ARV HAZIUZWI, ZIPO ZA KUTOSHA

Na Mwandishi Wetu, The Page

Serikali imewatoa hofu wananchi kuhusu dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV) na kusema zipo za kutosha na wala haziuzwi.

Taarifa iliyotolewa leo Februari 8,2025 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Afya, Roida Andusamile, imesema Serikali inaendelea kuweka mikakati thabiti na stahiki ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.

"Wizara ya Afya imebaini uwepo wa taarifa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vingine vya habari zikielezea uhaba wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV) kwamba watumiaji wanalazimika kununua.

"Taarifa hizi ni za upotoshaji na zimeleta hofu miongoni mwa wananchi na kusababisha baadhi ya wagonjwa kuomba kupewa dawa za muda mrefu kwa ajili ya akiba, jambo ambalo si sahihi na linaweza kuathiri utunzaji na matumizi sahihi ya dawa...hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa dawa hizi," amesema Andusamile. 

Ametoa rai kwa wananchi kupuuza taarifa hizo na kuendelea kutumia dawa kwa usahihi kama wanavyoelekezwa na wataalam wa afya ili kuzuia usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa na itaendelea kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

Powered by Blogger.