GODWIN MMBAGA: Mwanasiasa aliyefanya mengi tangu akiwa mdogo

Godwin Vincent Mmbaga.


Na Pendo Paulo

KILA binadamu ana ndoto na kiu ya kutaka kufika anapotaka kimaisha.

Wapo wanaoamua kufanya biashara za aina mbalimbali pia wapo wanaoamua kufanya shughuli tofauti na hiyo ili mradi akuze kipato.

Kuna wanaoanza harakati za kujikwamua kimaisha wakiwa na umri mdogo na wengine ukubwani.

Godwin Vincent Mmbaga ni mwanasiasa mzoefu aliyeianza safari yake ya kisiasa tangu akiwa na umri wa miaka 12 

Anasema aliianza safari hiyo akiwa darasa la tano katika Shule ya Msingi Muhimbili, iliyopo Upanga kwa kuchaguliwa nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Uendeshaji ya Chipukizi Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo ilitokana na nafasi yake ya Mwenyekiti wa Tawi Shule ya Msingi Muhimbili. 

"Nilipofika sekondari sikujishughulisha na siasa, lakini nilipokwenda kusoma DIT (Chuo cha Teknolojia) mwaka 1991 nilikuwa Katibu wa Tawi wa Jumuiya ya Vijana wa vyuo Tanzania na Korea (Jumuiya ya falsafa ya JUCHE) wanaosoma DIT na 1992 mpaka 1993 nikashika nafasi ya Mwenyekiti wa JUCHE," anaeleza Mmbaga.

Anasema sababu ya kuwania uongozi tangu akiwa mdogo ni kuwa na kiu ya kutaka kufika mbali siku zijazo kwa nafasi mbalimbali kwani anaamini uwezo anao.

Anaeleza kuwa sababu nyingine ni imani iliyojengwa na wanafunzi wenzake dhidi yake kutokana na kuongoza vyema katika nafasi mbalimbali za uongozi alizokuwa akichaguliwa akiwa masomoni.

Kwa mujibu wa Mmbaga mwaka 2002 hadi 2007 alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi - CCM tawi la Upanga Magharibi, mwaka 2003- 2007 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala. 

Mwaka 2007 hadi 2012 alichaguliwa kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Kata ya Upanga Magharibi pia alichaguliwa kuwa Mjumbe Baraza la Umoja wa Vijana Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam akiwakilisha Jumuiya ya Wazazi mkoa nafasi iliyomfanya awe Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo na baadaye mwaka 2010 aligombea udiwani katika Kata ya Upanga Magharibi (CCM) Ilala Dar es Salaam na kutumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2015.

Mwaka 2009 aliteuliwa kuwa mlezi wa tawi la CCM la Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) ambapo alikuwa mmoja wa waasisi wa shirikisho la matawi ya CCM ya vyuo vikuu wakiongozwa na Abdulrahaman Kinana. nafasi aliyoitumikia mpaka mwaka 2015.

Akiwa Diwani mwaka 2014 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Machinga Complex (soko la wafanyabiashara wadogo la Jiji) pia Meya wa Manispaa ya Ilala wakati huo Jerry Silaa, alimteua kuwa mratibu wa ofisi ya Meya wa Manispaa ya Ilala na Ofisi ya Meya wa Jiji la Kokkola, Finland katika ushirikiano wa urafiki kwa halmashauri hizo. 

Anasema baadaye mwaka 2016 alichaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Lembeni Wilaya ya Mwanga na mwaka 2020 aligombea Ubunge jimbo la Mwanga lakini hakufanikiwa kushinda.

Anaeleza kwamba hata hivyo baada ya kura za maoni, Chama cha Mapinduzi kilionyesha imani kubwa kwake na kumteua kuwa Meneja wa Kampeni Jimbo la Mwanga kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 na kufanikisha kunadi Rais, Mbunge na Madiwani ambapo CCM ilipata ushindi mkubwa. 

Akiwa Diwani wa Lembeni alifanikisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Kisangara, ujenzi wa nyumba za waganga katika Zahanati ya Kijiji cha Kiruru Mwanga ambazo zilikwama kwa muda mrefu kutokana na changamoto zilizokuwa zikikabili zahanati hiyo. 

Anasema alihamasisha uanzishwaji wa mradi wa mabweni ya wasichana Shule ya Sekondari Kisangara na kuwaondolea adha ya kutembea mwendo mrefu na kuwaepusha na mimba za utotoni. 

"Uanzishwaji wa mpango wa mabweni uliongeza ufaulu na kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata mimba," anasema Mmbaga.

Pia alifanikisha kuwepo kwa uwazi wa mapato na matumizi vijijini, kuhamasisha wananchi kujenga madarasa katika Shule ya Msingi Kiruru na Mbambua kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Vijiji. Pia alihuisha mahusiano kati ya taasisi zilizopo Kata ya Lembeni na serikali ya kata.

"Tuliongeza uwezo wa wenyeviti wa vijiji kujiamini katika nafasi zao, hii iliongeza mapato ya vijiji na takwimu zilionyesha ongezeko la vikao vijijini ambapo vijiji vingine walivuka malengo ya asilimia mia wakati hapo awali ilishuka mpaka asilimia 35 kwa baadhi ya vijiji, nilifarijika sana kutumikia Kata ya Lembeni," anasema Mmbaga.

Mmbaga alifanikisha upatikanaji wa mabati mengi kutokana na kiasi kidogo cha fedha kata iliyopokea toka Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga na kuomba ushirikiano kwa wadau mbalimbali waliopo jijini Dar es Salaam ambapo yalijenga Zahanati ya Kijiji cha Lembeni, mabweni ya wavulana Nyerere Sekondari pia darasa na ofisi ya walimu Shule ya Msingi Kisekibaha, Kijiji cha Lembeni. 

Pia alifanikisha mabadiliko ya mpango wa serikali wa maboresho ya kituo cha afya cha Kisangara na kuingiza mpango wa ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti ambapo awali hakikuwepo kwenye mpango wa 

Maboresho ya kituo cha afya cha Kisangara katika Kata yake ya Lembeni aliyokuwa akiiongoza.

Anasema alifanya kazi ya kuwatumikia wananchi wa Lembeni kwa miaka minne kisha alipumzika na kujikita zaidi katika kuimarisha shughuli zake za biashara nje na ndani ya nchi. 

Anasema mpaka sasa amejikita zaidi kwenye miradi yake ya biashara na ataona siku zijazo ikiwa itampendeza kurudi tena kwenye siasa ili kufikia ndoto zake za kuongoza Taifa katika maendeleo ya watu. 

Powered by Blogger.