UMEME NI MUHIMU KWA MAENDELEO YA TAIFA - DKT. KAZUNGU

*Akagua kituo cha umeme Kidatu

*Ataka usimamizi wa karibu kwa mkandarasi anayekarabati mtambo namba mbili

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Wizara ya Nishati imesema wanasambaza nishati ya umeme kwa ufanisi ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanapatikana kwa wananchi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. Khatibu Kazungu ameyasema hayo wakati alipotembelea kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu Mkoani Morogoro.

Amesema kituo hicho kinazalisha megawati 204 ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii hivyo watahakikisha wananchi wanapata nishati hiyo kwa uhakika.Amesema ni muhimu kusimamia miradi ya uzalishaji umeme ili kuwa na usambazaji wa nishati kwa ufanisi na kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanapata nishati hiyo.

"Wizara ya Nishati ina jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme ya uhakika kwa ajili ya kusukuma mbele shughuli mbalimbali za maendeleo," amesema Dk. Kazungu.

Dk. Kazungu amebainisha kuwa kituo cha Kidatu kilianza kuzalisha umeme tangu mwaka 1975 na sasa kinatimiza miaka 50 ya huduma hivyo Tanesco imetakiwa kufanya upembuzi yakinifu na kukikarabati ili kiendelee kuzalisha umeme kwa ufanisi.

Pia amekagua mtambo namba mbili unaofanyiwa ukarabati ulioanza Mei,2024 na unatarajiwa kukamilika Januari 2025.Dk. Kazungu ameiagiza Tanesco kuhakikisha mkandarasi anasimamiwa ili kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na mtambo huo uweze kuungana na mitambo mingine ambayo itaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme.

Naye Meneja wa Mradi wa kituo cha Kidatu, Manfred Lucas, amesema Tanesco itahakikisha kituo cha kufua umeme cha kidatu mitambo yake inakuwa katika hali nzuri na inafanya kazi muda wote ili kuchangia umeme wa kutosha kwenye gridi ya Taifa na kufanikisha azma ya Serikali.



Powered by Blogger.