RNK WAKABIDHI MISAADA KWA WATOTO YATIMA
KIKUNDI cha RNK kimekabidhi misaada mbalimbali ikiwemo vyakula kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu wanaolelewa katika Kituo cha Asante Community.
Wanakikundi hao wakiongozwa na Mwenyekiti Msaidizi, Joseph Asenga wamekabidhi misaada hiyo leo Desemba 14,2024 ikiwa ni maadhimisho ya mkutano wa mwaka wa kikundi hicho.
Akizungumza wakati wa kupokea misaada hiyo Mlezi wa Kituo hicho kilichopo Bombambili Kivule - Dar es Salaam, Magreth Edward, amesema kituo kina changamoto mbalimbali ikiwemo sare za shule, mabegi, saruji, vyakula na mahitaji mengine muhimu kwa watoto.
Amesema kituo kina jumla ya watoto 27 wakiwemo walemavu wa viungo wawili.
"Kituo kimefanikiwa kuwawezesha watoto kupata elimu ya msingi na sekondari bila udhamini wowote," amesema.
Magreth amewaomba wananchi na taasisi mbalimbali kuendelea kusaidia watoto hao kwani wana mahitaji makubwa ili waweze kuishi katika mazingira mazuri 
Mwenyekiti Msaidizi wa RNK, Joseph Asenga akipokea risala kutoka kwa mtoto Angel Hashim anayetunzwa katika Kituo cha Asante Community Kivule - Bombambili, Dar es Salaam.
