PROFESA MUTEMBEI AHIMIZA USOMAJI VITABU KUANZIA UTOTONI
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesema watoto wakijifunza kusoma vitabu wanavyovielewa kuanzia shule za awali vinavyochekesha na kuburudisha vitasaidia kuwa wagunduzi wakiwa na umri mdogo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtanzania wa Taasisi ya Confucius (CKD) na Mshauri Mtaalamu Lugha na Fasihi ya Kiswahili Chuo cha UDSM, Profesa Aldin Mutembei wakati akipokea vitabu nakala 43 sawa na vitabu 300 kutoka Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC).
Profesa Mutembei amesema kusoma vitabu ni tabia inayojengwa tangu utotoni hivyo wakisoma ambavyo vinachekesha vitawajengea kuwa na tabia ya kusoma mara kwa mara.
"Mtoto akijifunza kusoma tangu elimu ya awali ataelewa lugha na changamoto iliyopo watu hawasomi vitabu matokeo yake wanaangalia luninga pamoja na simu zao kwa kuangalia mitandao ya kijamii," amesema Profesa Mutembei.
Amesema watoto wadogo wakisomeshwa katika lugha ya kingereza, kichina na kifaransa hawatapenda kusoma hivyo wasomeshwe katika lugha wanayoielewa ili wakiwa wakubwa watasoma lugha nyingine ambazo ni muhimu kuwa nazo.
Pia amesema Kampuni ya CCCC imekuwa na utamaduni wa kutoa vitabu kwa ajili ya usomaji mbalimbali katika chuo hicho na miongoni mwa vitabu vilivyotolewa viwili vimeandikwa na Rais wa China.
Amesema rais huyo ameandika kitabu kinachoeleza utawala na kutoa fursa ya kuangalia upi bora kati ya utawala wa Magharibi na Mashariki.
Profesa huyo amesema historia ya China inakuwa kiuchumi, kitamaduni na kiteknolojia hivyo wanafunzi wanahimizwa kusoma utawala bora ili wajifunze mazuri waliokuwa nayo.
Amesema kitabu cha pili kilichoandikwa na rais huyo kinahusu mitandao ya barabara za biashara za Wachina zamani ilivyokuwa na sasa zimebadilishwa upya ili kuangalia namna gani biashara za Kichina na nchi zingine zinafanyika.
"Tanzania inafungua uwekezaji mkubwa ili tupate maendeleo hivyo, tunaposoma kitabu tunajifunza Wachina namna gani wanaendelea katika biashara, uchumi na teknolojia," amesema Profesa Mutembei.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CCCC, Li Xuecai, amesema mara ya kwanza waligawa vitabu katika chuo hicho na hii ni mara ya pili lengo likiwa kuimarisha urafiki kati ya Tanzania na China na kubadilishana tamaduni.
"Mwaka huu tumeadhimisha miaka 60 ya urafiki wa kidiplomasia hivyo, tuendelee kushirikiana ili kuleta maendeleo yatakayosaidia uchumi kukua," amesema.
Mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha UDSM, Betty Mongi, amesema chuo hicho kina programu ya kufundisha lugha ya Kichina hivyo ugawaji wa vitabu hivyo utasaidia kuongeza uelewa na kujua namna ya kuendana na tamaduni za Kichina.
