DK. JAFO MGENI RASMI KILELE CHA SIKU YA USHINDANI
Na Nora Damian, The Page
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wakati wa kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani.
Akizungumza leo Novemba 29,2024 wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), William Erio, amesema kilele kitafanyika Desemba 5 katika Hoteli ya Golden Tulip, Dar es Salaam.
Amesema katika kilele hicho kutakuwa na kongamano litakalohusisha magwiji wa ushindani na wanasheria ambao watapata fursa kujadili kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu na kuishauri FCC namna ya kuboresha shughuli zao.
Aidha amesema Desemba 2 hadi 3 kutakuwa na semina kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na wadau wa sheria na Desemba 4 elimu itatolewa kwa umma kupitia redio na luninga.
Kwa mujibu wa Erio, chimbuko la Siku ya Ushindani Duniani ni Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokutana mwaka 1980 ambalo lilipitisha kanuni mbalimbali zinazodhibiti vitendo vinavyofifisha ushindani katika biashara.
"Tanzania kama wanachama wa Umoja wa Mataifa wanaongozwa na sheria na sera zilizotokana na azimio hilo, tuna Sera ya Taifa ya Biashara ambapo ibara ya ushindani imo ndani yake," amesema Erio.
Mkurugenzi huyo amelishukuru Bunge kwa marekebisho yaliyopitishwa Septemba mwaka huu ambayo yataimarisha shughuli za biashara na ushindani nchini.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema 'Sera ya Ushindani na Kudhibiti Kukosekana kwa Usawa katika Uchumi’.
