DK. BITEKO ASISITIZA KUIMARISHWA USAFIRI WA MAJINI
Na Nora Damian,The Page
Naibu Waziri Mkuu na Waziri w Nishati, Dk. Doto Biteko ameishauri Jumuiya ya Mamlaka za Usimamizi wa Usafiri majini Barani Afrika kuungana ili kuimarisha usalama wa sekta ya usafirishaji majini.
Ametoa wito huo leo Novemba 29,2024 wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jumuiya ya Mamlaka za Usimamizi na Usafirishaji Majini Barani Afrika (AAMA) unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema hatua hiyo itachochea maendeleo ya uchumi katika nchi husika hivyo washiriki watumie mkutano huo kubuni na kupanga mikakati mipya ya mafanikio kupitia sekta hiyo.
“Kila mmoja atumie fursa ya mkutano huu kujiwekea malengo yatakayo tuwezesha kuboresha usalama na kuimarisha sekta ya usafirishaji wa majini,” amesema Dk. Biteko.
Naye Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema miongoni mwa masuala yanayohitaji kutiliwa mkazo ni pamoja na raslimali watu hususan vijana ambao watachagiza uendelevu na ukuaji wa sekta ya usafiri na usalama wa usafirishaji wa majini.
Amesema Tanzania imekuwa mstari wa mbele ikitekeleza maazimio ya uboreshaji sekta hiyo kwa kutekeleza miradi mikubwa inayolenga kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa miradi hiyo ya kimkakati ni pamoja na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa Reli ya Umeme kutoka Dar es Salaam - Morogoro - Dodoma ambayo mbali na kuongeza ufanisi katika usafirishaji pia inapunguza uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Masuala ya Baharini (IMO), Arsenio Dominguez, ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa kongamano na mkutano huo suala linaloonesha utayari wake katika uboreshaji wa sekta ya usafirishaji na usalama wa majini.
Amesema IMO itaendelea kuwezesha vikao hivyo vya kimataifa ili kujenga na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama ili kukabiliana na changamoto katika nchi husika.
Katibu Mkuu huyo amesema IMO ina program nyingi zinazohusu hifadhi ya mazingira na uwezeshaji kuelekea usawa wa kijinsia kwani wanawake wako nyuma katika masuala ya usafirishaji na usalama majini.


